Katika hali isiyotarajiwa na wengi, Katibu wa UVCCM wilaya ya Mbulu mkoani Manyara, Bi. Anna Gideria ameteuliwa na Chadema kuwa mbunge wa viti maalum.
Bi. Gideria amejiuzulu nafasi ya ukatibu na kukabidhi barua yake kwa mwenyekiti wa UVCCM mkoa wa Manyara, Bi. Regina Ndege baada ya kutangazwa majina ya viti maalum na jina lake kuwa katika orodha ya wabunge wa Chadema.
Akizungumzia hatua hiyo, Bi. Ndege alieleza kuwa Bi. Gideria alipoteza imani na CCM muda mfupi baada ya jina la waziri mkuu wa zamani, Frederick Sumaye kukatwa katika kinyang’anyiro cha kumtafuta mgombea urais kwa tiketi ya CCM.
Mwenyekiti huyo alieleza kuwa Bi. Gideria alikuwa ‘Team Sumaye’ na aliomba likizo ya mwezi mmoja baada ya jina la waziri mkuu huyo wa zamani kukatwa.
“Baada ya Sumaye kutoswa, alipoteza imani na CCM na ilipofika wakati wa kampeni mwezi Agosti aliandika barua ya kuomba likizo na kukabidhi ofisini kwa mjumbe wa kamati ya utekelezaji ya UVCCM wilaya ya Mbulu,” alisema Bi. Ndege.
Tukio hilo limewashtua wananchi wengi wa Wilaya ya Mbulu ambao walikuwa wanamuona Bi. Gideria kama kiongozi na mpambanaji wa CCM kuteuliwa kuwa mbunge wa Chadema.
Zipo hisia za wananchi wengi kuwa huenda alikuwa anatumiwa kuihujumu CCM wakati wa kampeni.