Hapa Kazi Tu ndiyo tunaweza kusema!! Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa mkoa wa Shinyanga imemfikisha hakimu mfawidhi Mwandu Sumay Luhaga (49)wa mahakama ya mwanzo Isungang’holo iliyopo kijiji cha Gimagi kata ya Shaghila wilayani Kishapu kwa kuomba na kupokea rushwa ya shilingi 500,000/= ikiwa ni sehemu ya shilingi 1,500,000/= kutoka kwa afisa mtendaji wa kijiji cha Mwajidalala wilayani humo.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Shinyanga Gasto Mkono,hakimu huyo amefikishwa katika mahakama ya wilaya ya Kishapu siku ya Jumatatu wiki hii kwa kosa la kuomba na kupokea rushwa kinyume na kifungu cha 15 cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2007.
Mkono alisema hakimu huyo anashtakiwa kwa kuomba shilingi 1,500,000/= na kupokea shilingi 500,000/= kama sehemu ya fedha hizo kutoka kwa Paschal Langula Bulugu ambaye ni afisa mtendaji wa kijiji cha Mwajidalala ili amfutie kesi yake namba 56/2015 iliyokuwa ikimkabili ya kumtorosha mtuhumiwa.
“Baada ya makubaliano kati ya hakimu na afisa mtendaji huyo tarehe 13 Novemba 2015,TAKUKURU iliweka mtego na kumfanikisha kumkamata hakimu na wakala wake Joel Jacob aliyetumika kupokea fedha hizo,na wote tumefungulia kesi ya jinai namba 33 ya mwaka 2015 kwa makosa ya kuomba na kupokea rushwa”,alifafanua Mkono.
Mkono aliongeza kuwa kutokana na TAKUKURU kupokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi dhidi ya hakimu Luhaga ya kuomba na kupokea rushwa,kubambikiza watu kesi na kuendesha kesi hizo bila kufuata utaratibu wa kimahakama walilazimika kufanya upekuzi nyumbani kwake ili kukusanya ushahidi wa kutosha juu ya tuhuma dhidi yake.
“Tulifanikisha kukuta majalada ya kesi yapatayo 202 ambayo kesi zake hazijasajiliwa mahakamani kwenye “case register” pamoja na vitu vingine mbalimbali ambavyo siwezi kuvitaja kwa sasa kwa faida ya uchunguzi”,alieleza Mkono.
Mkono alisema majalada hayo ya kesi yaliyokutwa nyumbani kwa hakimu huyo ni miongoni mwa kesi ambazo hakimu huyo alikuwa akiziendesha bila kufuata utaratibu kwa kumfungulia mtu kesi hapo hapo na kumhukumu hapo hapo bila kuita mashahidi wala kumpa nafasi ya kujitetea(kusikiliza upande wa mtuhumiwa.
Aidha alisema TAKUKURU mkoa wa Shinyanga inafanya uchunguzi juu ya tuhuma hiyo ya matumizi mabaya ya madaraka kinyume na kifungu cha 31 cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2007 na wakati wowote na jalada hilo likikamilika atafikishwa tena mahakamani kwa kosa hilo.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa TAKUKURU aliwataka wananchi kuwa makini na kukataa kutumiwa na watumishi wa umma kama wakala wa kupokea fedha za rushwa kwani kufanya hivyo wanaingia hatiani kwa mujibu wa sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2007.
Na Kadama Malunde- Malunde1 blog Shinyanga
Social Plugin