Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

Kimenuka!! WANANCHI WAKAMATA MUUGUZI KWA TUHUMA YA WIZI YA KUIBA DAWA KWENYE KITUO CHA AFYA,WALIOMKAMATA WASEMA WAPO TAYARI KUFA KWA MASLAHI YA UMMA




Kituo cha afya cha Kambarage katika manispaa ya Shinyanga,ambako ndiko kunadaiwa dawa zilizokamatwa zimetoka hapo



Muuguzi mkunga wa kituo cha afya Kambarage Joseph Nkila amekamatwa kwa tuhuma ya wizi wa dawa




Kaimu mganga mkuu wa manispaa ya Shinyanga Dkt Mhana Raphael akitoa taarifa kwa waandishi wa habari leo





Kaimu mkurugenzi wa manispaa ya Shinyanga Sande Deogratius akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo ambapo amewataka watumishi wa serikali kuzingatia maadili ya kazi zao pamoja na kufanya kazi kwa weledi kwani serikali inafanya juhudi kubwa za kuhakikisha kwamba inatoa huduma bora kwa wananchi .





Rashid Shaban ambaye ni mmoja wa wananchi 7 waliomkamata muuguzi huyo akiwa na dawa zinazodaiwa kuwa zimeibiwa katika kituo cha afya cha Kambarage.Amesema walikerwa na tabia za muuguzi huyo kuiba dawa wakati wananchi wengi wanakosa huduma za afya kutokana na kukosa dawa kwani ukienda katika kituo hicho cha afya unaambiwa hakuna dawa.Amesema baada ya kukamatwa kwa muuguzi huyo tayari wameanza kupata vitisho kwanini wamemkamata Joseph Nkila hivyo kuomba serikali ya rais Magufuli kuwalinda




Bwana Kagoma Hamis mkazi wa Ndala akizungumzia kuhusu namna walivyokamata dawa hizo kisha kuita polisi waliofika muda mfupi na kukamata dawa ambao walimkamata mtuhumiwa .Hamis aliiomba serikali kuwahakikishia usalama wa maisha yao kwani sasa wanapata vitisho baada ya kufichuo uovu huo.Amesema mara nyingi muuguzi huyu Joseph Nkila amekuwa akionekana na dawa za binadamu kinyume cha taratibu hivyo kutokana na uwepo wa serikali makini ya rais Magufuli wameamua kujitoa mhanga kuokoa jamii kwa kuamini kuwa serikali itawahakikishia usalama wao.


***********

Kauli ya Hapa Kazi Tu Imehamia kwa Wananchi!! Katika hali hali isiyokuwa ya kawaida baadhi ya wakazi wa kata ya Kambarage manispaa ya Shinyanga wamefanikisha kukamatwa kwa muuguzi mkunga katika kituo cha afya cha Kambarage mjini Shinyanga akituhumiwa kuiba dawa za kituo hicho.

Mashuhuda wa tukio hilo la aina yake wameiambia Malunde1 blog kuwa , limetokea jana majira ya saa tano asubuhi katika eneo la kituo cha afya Kambarage Shinyanga baada ya wananchi takribani saba kumtilia shaka muuguzi huyo aliyejulikana kwa jina la Joseph Nkila waliyemuona akitoka kituoni hapo akiwa ameficha mfuko waliohisi kuwa ni dawa za serikali.

Muuguzi amekamatwa na wananchi akiwa na kopo moja la dawa aina ya paracetamol na chupa mbili za dawa ya maji aina ya Erythromycin Syrup.

Wakisimulia jinsi walivyomkamata Rashid Shaban na Kagoma Hamis kati ya wananchi saba wanaofanya shughuli zao karibu na kituo hicho cha afya wameiambia Malunde1 blog kuwa kwa muda mrefu wamekuwa wakikerwa na mchezo mchafu wa muuguzi huyo ambaye mara nyingi amekuwa akionekana na maboksi ya dawa yenye nembo ya MSD na mara nyingi amekuwa akipaki gari lake kwenye eneo lao la kazi kisha kupandisha dawa hizo kwenye gari jingine na ndipo jana wakaamua kutimiza ile kauli mbiu ya mheshimiwa rais John Pombe Magufuli ya Hapa Kazi Tu.

Wamesema jana kama kawaida yake alifika eneo hilo kisha kushusha mfuko na kuuweka kwenye gari jingine na kumpa maelekezo dereva wa gari hilo kisha kuondoka haraka eneo hilo na kumuacha dereva wa gari hilo la pili,wakaamua kuzuia gari hilo wakammbana dereva akawaonesha dawa na kudai kuwa huwa wanazisafirisha kwenda kijijini.

Kaimu mganga mkuu wa manispaa ya Shinyanga Dkt Mhana Raphael amesema ni kweli muuguzi huyo amekamatwa na dawa hizo ambazo hazina nembo ya MSD ingawa uchunguzi wa awali wamebaini kuwa ni dawa za kituo hicho. 

Amesema muuguzi huyo ambaye amefanya kazi kwa zaidi ya miaka 12,siku hiyo hakuwa zamu bali alipeleka mgonjwa wake katika kituo hicho.

‘Sisi kama uongozi wa mkoa na halmashauri kwenye usimamizi wa dawa hatufanyi utani,tunaviachia vyombo vya dola vifanye kazi yake,kwa maana ya kuchunguza ili kubaini ukweli ili hatua stahiki zichukuliwe”,ameongeza Dkt Raphael.

Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga Justus Kamugisha amethibitisha kukamatwa kwa muuguzi huyu na kwamba bado wanaendelea kumhoji juu ya tukio hilo.


Na Kadama Malunde-Malunde1 blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com