KUHUSU MSAIDIZI WA LOWASSA KUKAMATWA NA POLISI

 
Jeshi la polisi linamshikilia mwanamkakati wa timu ya kampeni ya aliyekuwa mgombea urais wa Chadema

Mwanamkakati wa aliyekuwa mgombea wa urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Bashir Awale, amekamatwa na kuwekwa ndani katika Kituo cha Polisi cha Kati.
 
Habari zilizopatikana jana kutoka ndani ya timu ya kampeni ya mgombea wa Chadema, Edward Lowassa, zinasema kuwa Awale alikamatwa juzi jioni kwenye maeneo ya Mikocheni jijini Dar es Salaam.

Taarifa zaidi zinasema kuwa Awale alisimamamishwa na askari, ambao walimchukua kwenye gari lao huku wakilitelekeza gari lake kwenye maeneo hayo.
 
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Polisi Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova, aliliambia Nipashe atalizungumzia suala hilo leo pamoja na mambo mengine.
 
“Nimewaagiza vijana wangu waniandalie taarifa juu ya suala hilo. Nitalizungumzia jambo hilo kesho (leo) pamoja na mambo na mengine,” alieleza Kamishna Kova, ambaye hakutaka kuingia kwa undani wakati alipohojiwa na gazeti hili kuhusiana na suala hilo.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili unaonyesha kwamba kukamatwa kwa Awale kunahusishwa na masuala ya Uchaguzi Mkuu uliomalizika hivi karibuni kutokana na ukaribu wake na Lowassa.
 
Lowassa alishindwa kwenye uchaguzi wa urais baada ya kushika nafasi ya pili kwa kupata kura 6,072, 848 sawa na asilimia 39.97 wakati mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk John Magufuli aliibuka mshindi kwa kupata kura 8,882,935 sawa na asilimia 58.46.
 
Awale alikuwa miongoni mwa viongozi waandamizi kwenye timu ya kampeni ya Lowassa tangu wakati alipokuwa mwanachama wa CCM.

Lowassa alipoachana na CCM na kujiunga na Chadema, Julai 28 mwaka huu, Awale alikuwa miongoni mwa watu waliofuatana naye.
 
Awale alikuwa miongoni mwa watu waliofuatana Lowassa siku anatambulishwa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, baada ya kujiunga rasmi na chama hicho.
 
Kabla ya kuingia kwenye masuala ya siasa, Awale alikuwa Ofisa Mkuu Mtendaji wa Benki ya Stanbic nchini Tanzania kabla ya kuachia ngazi mwaka 2013.
 
Aliiongoza benki ya Stanbic kuanzia mwaka 2006, lakini kabla ya hapo alikuwa akifanya kazi katika Benki ya Citibank.

Tangu alipoachana na Stanbic, Awale alikuwa miongoni mwa wanamkakati waandamizi wa Lowassa tangu alipokuwa akiwania kugombea urais kwa tiketi ya CCM.
 
Lowassa alipokatwa jina lake CCM na kujiunga na Chadema, Awale alikuwamo kwenye timu ya kampeni akiwa miongoni mwa viongozi waandamizi.
 
 
Pamoja na kuwemo kwenye timu ya kampeni, pia ni anachukuliwa kama miongoni mwa wasaidizi na washauri muhimu wa Lowassa.

Kukamatwa kwa Awale kunakuja baada ya hivi karibuni vijana wanane waliokuwa wakisaidia kazi ya kujumlisha kura za Lowassa kwenye kituo cha vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kukamatwa na kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za kujumlisha matokeo ya kura za urais katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu.

NIPASHE

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post