LOWASSA KUMNADI MGOMBEA UBUNGE JIMBO LA ARUSHA MJINI GODBLESS LEMA JUMAMOSI HII..."LOLOTE LAWEZA KUTOKEA KWA UWEZO WA MUNGU" -LEMA

Aliyekuwa mgombea wa urais wa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa anatarajiwa kupanda jukwaani Jumamosi kumuombea kura mgombea wa ubunge wa Chadema Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema.

Akizungumza katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni za ubunge katika jimbo hilo uliofanyika Soko Kuu jana, Lema alisema Lowassa atazungumza na Watanzania na kuwashukuru pia kwa kura nyingi walizompa.

Awali, mbunge mteule wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ alieleza kuwa Lowassa na viongozi wa Chadema watatoa tamko zito siku hiyo na kuwataka wakazi wa Arusha na Watanzania kutega masikio.

Lema ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, aliwataka wakazi wa Arusha, kutokatishwa tamaa na kuendelea kuwa na huzuni kutokana na matokeo ya urais yaliyotangazwa na kuwa bado kuna harakati za chama hicho kusaka haki.

“Ndugu zangu msikate tamaa, tumesikia wengine wametupa shahada zao, hapana, kazi ndiyo imeanza na lolote linaweza kutokea kwa uwezo wa Mungu,” alisema.

Alisema huzuni ya matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), haipo kwa wananchi tu, bali hata wajumbe wote wa kamati kuu.

“...Kwenye kikao cha kamati kuu, kuna wajumbe walimuomba Lowassa atoe tamko... kama angetoa tamko la kupinga matokeo na kukubali watu kuingia mitaani, Tanzania ingekuwa imeingia katika machafuko makubwa.

“Tunaendelea kutumia taasisi za kimataifa kudai haki, ndiyo sababu mnaona Zanzibar wameshindwa kujitangazia matokeo, hii ni kazi kubwa ya Ukawa,” alisema.

Katika mkutano huo, Lema alieleza njama alizosema zinapangwa kumnyima ushindi na akaonya kuwa hatakuwa tayari kuona ameshinda lakini mwingine akatangazwa kushinda.

“Najua Arusha nitashinda kwa kura nyingi, lakini kama wakitaka kunipora ushindi sitakubali,” alisema Lema.

Aliwaomba wakazi wa Arusha kujitokeza kwa wingi Desemba 13 kumpigia kura nyingi, ili pia kuwezesha Chadema kupata viti viwili zaidi vya wabunge wa viti maalumu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post