Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MAHAKAMA KUU KANDA YA MWANZA KUTOA UAMUZI JUU YA MWILI WA ALIYEKUWA MWENYEKITI WA CHADEMA MKOA WA GEITA



Mahakama kuu kanda ya Mwanza imetupilia mbali mapingamizi ya kisheria yaliyowekwa na kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza na mwanasheria mkuu wa serikali, kwamba mtoa maombi katika kesi hiyo ya madai namba 10 ya mwaka 2015 Bw.Charles Lugiko ambaye ni baba mdogo wa marehemu Alphonce Mawazo hana uhalali wa kisheria wa kuwasilisha maombi hayo kwa vile yeye si baba mzazi wa marehemu. 


 
Jaji wa mahakama kuu kanda ya Mwanza Mh. Lameck Mlacha ametupilia mbali hoja za mawakili wa serikali Emily Kiria na Seth Mkemwa ambao walitaka kusiwe na kesi ya msingi kwa kuwa mtoa maombi hakuwasilisha mahakamani hapo hoja za kubishaniwa kwenye shauri hilo, huku upande wa utetezi unaoongozwa na mawakili watatu wa chama cha demokrasia na maendeleo John Mallya, James Ole Millya na Paul Kipeja ukijibu hoja hizo kwamba katika hatua hiyo masuala ya kubishaniwa hayana sababu ya kuletwa kwa kuwa ni hatua ya awali sana. 
 

Kuhusu uhalali wa kisheria wa baba mdogo wa marehemu, majibu yalikuwa kwamba baba mdogo kwa kuwa ndiye aliyemlea marehemu Mawazo tangu akiwa na miezi miwili tangu kuzaliwa kwake, kwa mila za kitanzania anayo mamlaka na uhalali wa kisheria wa kuwasilisha maombi hayo.

Mahakama imekubaliana na hoja za mawakili wa mtoa maombi na kuamua kuruhusu kesi ya msingi kufunguliwa kama ilivyoombwa na kutupilia mbali mapingamizi ya mlalamikiwa wa kwanza kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza na mwanasheria mkuu wa serikali.

Nje ya mahakama hiyo, wakili wa mlalamikaji John Mallya amezungumza na waandishi wa habari kuelezea hatua zaidi zinazofuata baada ya mahakama kuu kanda ya Mwanza kuruhusu kesi hiyo ambayo imevuta hisia za mamia ya wakazi wa jiji la Mwanza kuanza kusikilizwa hapo kesho chini ya hati ya dharura.

Uamuzi huo mdogo wa jaji wa mahakama kuu kanda ya Mwanza Mh. Lameck Mlacha umepokelewaje na mwenyekiti wa taifa wa chama cha demokrasia na maendeleo (Chadema) Mh.Freeman Mbowe.

Via>>ITV

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com