Watu wanne ambao ni wachimbaji wadogowadogo wamefariki dunia baada ya kufukiwa na kifusi katika eneo la Prospect 30 lililopo eneo la Mgusu wilayani Geita linalomilikiwa na Mgodi wa Dhahabu( GGM) walipokwenda kutafuta dhahabu.
Malunde1 blog ilifika katika eneo hilo liloko katika kijiji cha Mgusu na kukuta wachimbaji wakiwa na dhana duni wakichimba na kumuokoa mwenzao wa tano ambaye alikuwa hajatolewa katika shimo hilo.
Wakizungumza na Malunde1 blog baadhi ya wachimbaji hao walisema tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo majira ya saa sita usiku ambapo wenzao walifukiwa na kifusi wakiwa katika shimo hilo huku wakiomba kutafutiwa maeneo ya kuchimba na kuacha kuwa kama wavamizi kwenye nchi yao.
Walisema hali duni ya maisha huwalazimu kufanya shughuli hiyo hatarishi bila kuzingatia usalama ambapo wameiomba serikali kusaidia kundi la wachimbaji wasio rasmi ili wapate eneo la kuchimba kwa usalama.
“Wenzetu wamekufa kwa kufukiwa na kifusi katika mashimo ya Mgodi wa GGM siyo kwamba tunavamia ,sisi ni wazawa wa Mkoa huu ,maeneo yote yamekwisha kuporwa na wakubwa,kila unakogusa ni kupigwa mabomu na kuambiwa wewe ni mvamizi tutaishi kwa namna gani”,alihoji Wilson.
Kaimu afisa madini mkazi mkoa wa Geita Fabian Lucas alisema eneo hilo linamilikiwa na kampuni ya uchimbaji ya mgodi wa dhahabu wa Geita na kwamba wachimbaji hao wasio rasmi wameingia kuchimba eneo hilo kinyume na sheria hivyo kuwataka kujiunga katika vikundi ili waweze kupatiwa maeneo na leseni kihalali.
Lukas alisema watu hao waliingia kinyume na sheria katika Mgodi huo na ni wavamizi kama wavamizi wengine .
Meneja mahusiano ya jamii wa mgodi wa dhahabu wa Geita Manase Ndoroma amewataka vijana wanaojishughulisha na uchimbaji kuzingatia usalama wa miamba wanayotafuta dhahabu hasa msimu huu wa masika kutokana na eneo lenyewe kuwa na mwamba laini.
Jeshi la polisi mkoa wa Geita limethibitisha kutokea kwa tukio hilo na uchunguzi unaendelea.
Waliokufa katika Mgodi huo ni Emmanuel Emmanuel, Lucas Deus, Maliatabu Budonyanga , Clement Richard na Baraka Katunzi ambaye mwili wake bado haujapatikana.
Wachimbaji wadogo wa mkoa wa Geita wamekuwa wakihangaika kutafuta pa kuchimba huku maeneo yote yakiwa yameporwa na watu wenye fedha zao.
Na Valence Robert-Malunde1 blog Geita