Mwenyekiti wa taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mh. Freeman Mbowe ameongoza mamia ya wakazi wa mkoa wa Geita katika mazishi ya aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho mkoani humo Alphonce Mawazo yaliyofanyika leo kijijini kwao Chikobe wilayani Geita.
Mazishi hayo yalitanguliwa na waombolezaji kutoa heshima zao za mwisho katika uwanja wa kijiji cha Chikobe licha ya mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha kuanzia majira ya asubuhi.
Viongozi wengine waliohudhuria mazishi hayo ni pamoja na aliyekuwa mgombea urais wa Chadema akiungwa mkono na vyama vinavyounda umoja wa katiba ya wananchi (UKAWA) Mh. Edward Lowassa, waziri mkuu mstaafu wa serikali ya awamu ya tatu Mh. Fredrick Sumaye, makamu mwenyekiti wa Chadema upande wa Zanzibar Said Issa Mohamed na kaimu katibu mkuu wa Chadema Salum Mwalimu.
Kabla ya mazishi kufanyika, Mh. Mbowe aliwapa neno la faraja wafiwa.
Ilipotimu majira ya saa tisa na dakika ishirini na moja alasiri jeneza lililoubeba mwili wa marehemu Alphonce Mawazo likashushwa kaburini na vijana wa kikosi cha ulinzi wa Chadema maarufu kama Red Brigade ikiwa ni siku ya kumi na saba toka alipouawa kikatili kwa kukatwa na mapanga na watu ambao bado hawajatiwa nguvuni na jeshi la polisi.
Via>>Itv
Social Plugin