Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MASHINE ZA MUHIMBILI ZAHARIBIKA TENA...WANANCHI WASEMA SERIKALI HAIKO MAKINI NA AFYA ZA WATANZANIA




Siku chache baada ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kutengeneza mashine ya MRI (Magnetic Resonance Imaging) na kuanza kufanya kazi kwa takribani siku mbili, imeharibika tena.

Hatua ya Muhimbili kutengeneza kifaa hicho kichositisha kufanya kazi kwa miezi miwili, ilifuatia ziara ya Rais, John Maguful, aliyoifanya Novemba 9 mwaka huu kwa kushtukiza katika hospitali hiyo ya taifa na kuagiza itengenezwe pamoja na ile ya CT- Scan ndani ya siku 14.


Mkuu wa Kitengo cha Mawasilano ya Umma na Huduma kwa Wateja wa Muhimbili, Aminiel Aligaesha, jana alisema kipimo hicho kilisita kufanya kazi Novemba 13, mwaka huu.

Alisema mashine hiyo baada ya kufanyiwa matengenezo ilianza kufanya kazi Novemba 11 na 12 mwaka huu na kutibu jumla ya wagonjwa 26 kabla ya kuanza kuonyesha hitilafu.

“Mtakumbuka mapema wiki iliyopita tuliwatangazia wananchi kuwa huduma za MRI zimeanza kutolewa baada ya mashine hiyo kutengenezwa na kuanza kufanya kazi, lakini sasa tumesimamisha huduma hiyo tena baada ya kuleta hitilafu kwa ajili ya kufanyiwa matengenezo,” alisema.

MATENGENEZO
Aligaesha alisema uongozi wa Muhimbili uliwasiliana na kampuni ya Philips ambayo ina mkataba wa kufanya matengenezo ya mashine za MRI na CT-Scan ili kuondoa hitilafu hizo.

“Baada ya kuchunguza kwa kina mafundi wamebaini hitilafu kwenye mashine ya MRI, kifaa kiitwacho RF Amplifier kimeharibika na inabidi kiwekwe kingine,” alisema.

Aligaesha alisema kazi ya kifaa hicho ni kuipatia mashine hiyo mawimbi ya sauti (radio frequency) ambayo yanahitajika katika sehemu nyingine za mashine kuiwezesha kufanya kazi vizuri.

Alisema vifaa hivyo vimeagizwa kwa hati ya dharura na kwamba vinatarajiwa kuingia nchini katikati ya wiki hii.
Alisema mashine hiyo pia ilikuwa na uwezo wa kutibu watu 10 hadi 15 kwa siku kutokana na kufanya kazi taratibu kwa kuhudumia mgonjwa mmoja kwa dakika 40.

CT-SCAN
Kwa upande wa CT-Scan, alisema uchunguzi ulibaini inahitilafu kwenye vifaa viwili, kifaa kiitwacho Image re-constructor (server) kinachohusika kutengeneza picha na kifaa kiitwacho Inverter Power Supply kinachohusika kupeleka umeme wenye kiwango kinachohtajika chenye mashine.

“Vifaa vyote hivi havipatikani nchini na vimeagizwa kwa hati ya dharura nchini Uholanzi kwa mtengenezaji wa mashine hizi ambaye ni kampuni ya Philips na vinatarajiwa kuwasili ndani ya wiki hii. Tunaomba wateja wetu wawe watulivu wakati huu ambao suala hilo linashughulikiwa,” alisema Aligaesha.

Pia alisema mashine hiyo ya CT-Scan ina uwezo wa kutibu wagonjwa 40 hadi 45 kwa siku na kwamba wanatarajia kuongeza mashine hizo na ambazo zina uwezo mkubwa zaidi.

Kuhusu huduma za matibabu kwa wagonjwa watakaotakiwa kufanyiwa kipimo hicho, Eligaesha alisema watagharamia huduma hizo katika hospitali binafsi kwa utaratibu maalum ulioandaliwa.

“Kwa wagonjwa wa dharura tumeagiza mwanasheria wetu kuandaa hati ya makubaliano kwa ajili ya kuwapatia matibabu katika hospitali binafsi wakati huu mashine zikiwa zinatengenezwa,” alisema.

SABABU ZA KUTOFANYA KAZI
Aligaesha alisema sababu za mashine hizo kutofanyiwa matengenezo kwa kipindi cha miaka miwili ni kutokana na kampuni ya Philips kuidai serikali zaidi ya dola za Marekani 400,000.

“Kwa sasa tunachofanya ni serikali kulipa deni hilo na tunatarajia kumaliza deni hilo rasmi ifikapo Februari mwakani,” alisema.

WANANCHI WALIA
Kwa upande wa wananchi waliotoa maoni yao kuhusiana na kuharibika kwa mashine hiyo kwa mara nyingine, walisema serikali inapaswa kujipanga ili kuhakikisha inatoa huduma bora na muhimu kwa wateja.

Ashron Maiga, alisema kipimo kama hicho kutofanya kazi kwa muda wa miezi miwili ni wazi kuwa serikali haiko makini na afya za Watanzania.

“Kipimo hicho kimefanya kazi siku mbili na kimeharibika tena, huku nikutuumuza sisi wananchi, kuna haja ya mashine hizo kuongezwa na kuletwa zilizo salama zaidi,” alisema Maiga.

Naye Harieth Dandu, alisema wananchi masikini ndiyo ambao wamekuwa wakipoteza maisha kila siku kutokana na kukosa huduma hizo.

“Serikali inadai kila siku matibabu bure lakini mashine kama hizi siyo bure, sawa tunachangia kidogo lakini hata hizo za kuchangia zimekufa, serikali ihakikishe inazitengeneza ili maisha ya Watanzania masiki yapone,” alisema.

CHANZO: NIPASHE

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com