Mwanafunzi wa Chuo cha Taasisi ya Teknolojia Tanzania (DIT), Benedict Ngonyani
Mwanafunzi wa Chuo cha Taasisi ya Teknolojia Tanzania (DIT), Benedict Ngonyani anayetuhumiwa, kusambaza taarifa katika mtandao wa kijamii wa Facebook kuwa Mkuu wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Jenerali Davis Mwamunyange amelishwa sumu amepata dhamana.
Uamuzi huo ulifikiwa jana na Hakimu Mkazi Respicious Mwijage wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, baada ya kutengua hati ya kuzuia dhamana iliyowasilishwa mahakamani hapo na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kutokana na kutokuwapo na sababu za msingi za kuzuia dhamana hiyo.
Alisema si kwa upande wa mashtaka wala mtuhumiwa, hakuna aliyeieleza kama mtu anayedaiwa kuwekewa sumu kuwa ni Mwamunyange ambaye ameonekana hadharani au mahali alipo.
Hakimu Mwijage alisema kama wangekuwa wameieleza mahakama kwamba sehemu anapoishi Mwamunyange hajawahi kuonekana wala hadharani, angeweza kutofautisha kuhusu suala la usalama na maslahi ya taifa “nafikiri hapa kungekuwa hakuna kesi”.
Pia, alisema mshtakiwa ni mwanafunzi na shtaka analoshtakiwa nalo linadhaminika kwa hiyo haoni haja ya kukosa masomo yake ya darasani.
Mwijage alisema sio kila shtaka linawekewa zuio, upelelezi umeshakamilika na haoni haja ya kuzuia dhamana ya mshtakiwa.
Mshtakiwa alitakiwa awe na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya shilingi milioni tano kila mmoja.
Awali, Mwijage alitoa siku saba kwa DPP kuondoa zuio la dhamana kwa mshtakiwa kutokana na kutokuwepo na maelezo ya kutosha, “Natoa siku saba kwa DPP kuondoa zuio la dhamana ya Ngonyani, vinginevyo nitatoa uamuzi wangu.”
Mutakwao alidai kifungu cha 148 (4), kinaeleza wazi kuwa mwenye mamlaka ya kuondoa hati ya zuio la dhamana ni DPP mwenyewe. Awali, Mwijage alisema.
Ilidaiwa Septemba 25, 2015 mshtakiwa akiwa Dar es Salaam alisambaza taarifa za uongo kinyume cha Sheria ya Makosa ya Mtandao kifungu cha 16 ya mwaka 2015.
Ngonyani anadaiwa siku hiyo hiyo alisambaza taarifa kuwa Mwamunyange amelishwa sumu huku akijua taarifa hizo ni za uongo na zilikuwa na lengo la kupotosha umma. Baada ya mshtakiwa kusomewa shtaka hilo alikana kuhusika.
CHANZO: NIPASHE