UMOJA wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), umesema mipango yao ya kutomruhusu Rais Dk. John Magufuli kulihutubia Bunge akiwa na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, imefanikiwa.
Mwenyekiti wa Umoja huo, Freeman Mbowe, alisema jana kuwa walimua kuzuia Rais Magufuli asihutubie Bunge kwa vile Dk. Shein, muda wake wa kuwa rais ulikwisha tangu Novemba 2 mwaka huu kwa hiyo hakustahili kuhudhuria Bunge hilo.
Alisema kuwa waliamua kufanya vile wakiamini kuwa ilikuwa sehemu muafaka ya kufikisha kilio chao kutokana na wageni mbalimbali waliohudhuria mkutano ule, wakitokea katika nchi za jumuiya ya kimataifa.
“Tulishangaa kumuona Dk. Shein, Pandu Amiri Kificho na Makamu wa Pili wa Rais wakiwa ndani ya Bunge wakati kikatiba hawana uhalali,” alisema Mbowe.
Alisema, baada ya kitendo kile hivi sasa umoja wa vyama hivyo, unatarajia kukutana ili kupeana mikakati ya kuendeleza mapambano ya ndani na nje ya nchi ya kudai haki.
“Uchaguzi wa Zanzibar hauwezi kutenganishwa kikatiba au kisiasa na uchaguzi mkuu wa Jamhuri ya muungano,” alisema Mbowe.
Mbowe alisema Ukawa hawako tayari kuinajisi Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuruhusu viongozi wasio halali kuingia bungeni.
Aidha, Mbowe alisema walitaka shughuli ya ufunguzi rasmi wa Bunge isitishwe kwa sasa na kuahirishwa hadi hapo Rais halali aliyechaguliwa na wananchi wa Zanzibar, Seif Sharrif Hamad, atakapotangazwa rasmi na kuapishwa.
Naye Mwenyekiti Mwenza, James Mbatia, alisema haijawahi kutokea katika historia ya Bunge tangu nchi hiyo ilipopata uhuru kwa vyombo vya dola kuingia ndani ya bunge na kuwatoa wabunge kwa nguvu.
“Wakati sisi tunatafuta majadiliano mezani ilikumaliza mgogoro huu wenzetu Chama Cha Mapinduzi (CCM), wameamua kutumia majeshi kukandamiza demokrasia,” alisema Mbatia.
Mbatia alisema kuwa hawatakaa kimya bali wataendelea kupigania matakwa ya wananchi hususan kwa upande wa Zanzibara.
“Kuna mambo mengi yanafanywa hovyo na CCM na wapinzani wamekuwa wakivumilia kwa sababu ya kumpenda mama Tanzania lakini hivi sasa wasijaribu kuharibu amani, utulivu na mshikamano uliopo,” alisema.
Mbatia, alisema kwa kawaida mtu anapodhulumiwa haki yake kila mara matokeo yake anachoka kwa hiyo kuna siku ataifuta haki yake hata kwa kusababisha kumwaga damu.
Naye Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu alisema Umoja wa Katiba ya Wanachi (Ukawa ) wamesikitishwa na kitendo cha serikali ya CCM kuonesha wazi jinsi walivyobaka na kuikanyaga demokrasia nchini.
Alitoa kauli hiyo aipokuwa akizungumza na mwandishi wetu muda mfupi baada ya kutoka bungeni baada ya kufukuzwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai baada ya wabunge wa umoja huo kupinga kitendo cha kuruhusiwa kwa Rais wa Zanzibar kuwa sehemu ya Bunge.
Lissu alisema imeonesha wazi kuwa serikali ya CCM ilivyo kuwa ikitumia mabavu ya kuvunja sheria waziwazi sambamba na kuvunja kanuni za bunge jambo ambalo ni hatari kwa afya ya nchi.
Akizungumzia kutoka kwao nje ya ukumbi wa Bunge alisema serikali ya CCM kwa kutumia kiti cha Spika walionekana kupanga mbinu chafu za kuwazima wabunge wa Ukawa ili wasiweze kufikisha hoja zao mbele za wananchi kupitia bunge hilo.
“Unaweza kuona kwamba serikali ya CCM inavyoweza kuvitumia vibaya vyombo vya dola, kwa utaratibu jinsi ulivyo ili kuruhusu watu waingie katika ukumbi wa bunge ni lazima kutengua kanuni ili watu waeze kuingia lakini kutokana na uovyo na ujinga mkubwa wa serikali ya CCM, ambayo haizingatii sheria na katiba imeweza kuleta askari wengi pamoja na majeshi kwa ajili ya kukabiliana na upinzani.
“Jambo kubwa na baya zaidi na la ajabu ni pale ambapo askali waliovaa magwanda ya polisi na jeshi wakiwa na silaha za moto walivyoweza kuingia katika ukumbi wa bunge kwa misingi ya kutaka kukabiliana na wabunge wa upinzani.
“Jambo hapa ni kwamba hata wao wanajua kuwa Dk. Shein siyo rais halali wa Zanziba lakini kwa ubishi wao wanalazimisha kufanya hivyo na kutokana na hali hiyo ndiyo maana serikali imekuwa ikitumia vyombo vya dola kwa ajili ya kuthibiti wabunge wa Upinzania ambao wametumwa na Umma wasitoe mawazo yao,” amesema Lissu.
Mbali na hilo alisema pamoja na kuwa walizuiliwa kuendelea na bunge, kwa ajili ya kuwasilisha hoja zao kwa watanzania lakini watatumia mbinu nyingi za kufikisha ujumbe kwa jamii kwani kwa sasa kuna kila mikakati ya kuhakikisha wanataka kuuzima upinzani.
Akizungumzia kuhusu kanuni za bunge kwa sasa alisema kama ilivyo katiba ya sasa ilivyo na makosa kibao ndivyo na kanuni za bunge zinavyotakiwa kurekebishwa kwani kuna makosa mengi zaidi.
Kwa upande wao wabunge wa Zanzibar walisema ni dhambi kubwa kwa Dk. Ali Mohamed Shein kuenedelea kung’ang’ania kukaa madarakani wakati muda wake umeisha jambo ambalo linaonesha wazi kuwa ni matumizi mabaya ya madaraka na dola yake.
“Inasikisha zaidi kuona jinsi Rais wa Zanzibar alivyokuwa siyo muungwana anajua kabisa kwamba hakushinda uchaguzi, lakini ikumbukwe wakati wa kuvunja baraza la wawakirishi wabunge wa CCM walimkataa Maalim Seif Shariff Hamad kama makamu wa kwanza wa rais asiingie katika bunge.
“Lakini kwa uungwana wa kiongozi huyo aliondoka wala hakuhudhuria kikao hicho lakini jambo la kushangaza huyu Dk. Shein amekomaa sasa inafikia hatua anazomewa bila kuwa na aibu sasa huo ni uongozi gani na anamuongoza nani,” amesema.
“Tunamuuliza Rais Magufuli, ni nani akapeleka vifaru na kuongeza askari wengi katika nchi za Zanzibar na ni kwa sababu gani.
“Kwa sasa hali ya Zanzibar si shwali kwani kila jambo sasa limelala kwani hata watalii hawaji kama ilivyokuwa mwanzo, mbali na hilo kuna hali ya sitofahamu ni kwani nguvu nyingi ya vyombo vya dola inaelekezwa Zanzibar,” alisema mmoja wa wabunge wa Zanzibar.
Via>>Mpekuzi blog
Social Plugin