Dawa zikiwa katika stoo ya kituo cha afya cha Kambarage mjini Shinyanga-picha na Kadama Malunde-Malunde1 blog
Katika hali isiyokuwa ya kawaida wananchi mjini Shinyanga wamemkamata muuguzi mkunga Joseph Nkila wa kituo cha afya Kambarage katika manispaa ya Shinyanga akiwa na dawa za serikali akizisafirisha kusikojulikana kinyume na taratibu katika eneo la kituo hicho kisha kumfikisha kituo cha polisi.
Muuguzi mkunga Joseph Nkila ambaye ni mfanyakazi wa kituo cha afya Kambarage alikamatwa Novemba 24,2015 saa tano asubuhi na wananchi akiwa na kopo moja la dawa aina ya paracetamol na chupa mbili za dawa ya maji aina ya Erythromycin.
Wakisimulia jinsi walivyomkamata Rashid Shaban na Kagoma Hamis kati ya wananchi saba wanaofanya shughuli zao karibu na kituo hicho cha afya walisema kwa muda mrefu wamekuwa wakikerwa na mchezo mchafu wa muuguzi huyo ambaye mara nyingi amekuwa akionekana na maboksi ya dawa yenye nembo ya MSD kwenye gari lake.
“Amekuwa akija na gari lake hapa na dawa,kisha kupakia dawa hizo kwenye gari jingine,amekuja hapa na gari kama kawaida akiwa na mfuko,kisha akauingiza kwenye gari la pili na kumpa maelekezo kwa dereva na kuondoka,ndipo tukaamua kuzuia gari hilo la pili tukakuta dawa,tukaita polisi,wakaja kukamata dawa hizo”,walieleza wananchi hao.
Walisema baada ya kuzuia gari hilo walimbana dereva akawaonesha dawa na kudai kuwa hajui chochote kuhusu dawa hizo na kwamba huwa wanazisafirisha kwenda kijijini.
Hata hivyo mbali na kufanikisha kukamata kwa dawa hizo walisema tayari wameanza kupewa vitisho na ndugu na marafiki wa muuguzi huyo ambaye anashikiliwa na jeshi la polisi huku wakidai kuwa wapo tayari kufa kwa maslahi ya umma.
“Huu mchezo anaufanya mara nyingi,akina mama wanakosa huduma muhimu za afya,tumeamua kujitoa muhanga kusaidia watu wengi,watu wanakufa kwa kukosa dawa kwa sababu ya watu wachache kama hawa,ukienda kwenye kituo cha afya unaambiwa dawa hakuna,hii haiwezekani,tunaomba serikali ichukue hatua kali”,waliongeza.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari Kaimu mganga mkuu wa manispaa ya Shinyanga Dkt Mhana Raphael alisema ni kweli muuguzi huyo ambaye ni mfanyakazi wa kituo cha afya Kambarage na ana miaka 12 kazini amekamatwa na dawa hizo ambazo hazina nembo ya MSD ingawa uchunguzi wa awali wamebaini kuwa ni dawa za kituo hicho.
“Muuguzi huyu amekamatwa na wananchi baada ya ile mitego tuliyokuwa tumeiweka,wakampeleka kituo cha polisi,mpaka sasa upelelezi wa kesi unaendelea,ingawa taarifa za awali zinaashiria kuwa ni kweli kakamatwa na dawa kutoka kituo hicho isipokuwa tu hazina nembo ya MSD lakini uchunguzi wa awali unaonesha kuwa ni dawa za kituo hicho cha afya”,alieleza Dkt Raphael.
‘Sisi kama uongozi wa mkoa na halmashauri kwenye usimamizi wa dawa hatufanyi utani,tunaviachia vyombo vya dola vifanye kazi yake,kwa maana ya kuchunguza ili kubaini ukweli ili hatua stahiki zichukuliwe kwa mujibu wa sheria ili liwe fundisho kwa watumishi wengine wenye tabia za kuiba dawa za serikali na kuwakosesha huduma wananchi”,aliongeza Dkt Raphael.
Amesema tayari wanaendelea na zoezi endelevu la ukaguzi kwenye vituo vyote ili kubaini kama kuna upotevu usio wa lazima unaotokana na watu wadanganyifu na kuhakikisha kuwa unadhibitiwa kwani wapo watu ambao kinyume na maadili yao ya kazi yao wanachukua dawa vituoni na pengine kuchukua kwa ajili ya matumizi yao binafsi au kufanya biashara nje ya utaratibu
“Kama wapo watumishi wa aina hii,sisi na kikosi chetu cha uendeshaji tumekuwa tukichukua hatua ili kuhakikisha kuwa dawa hazipungui vituoni,na katika mkoa wa Shinyanga tumekuwa na mafanikio hatujapungukiwa na dawa isipokuwa kuna watu wachache wanajaribu kurudisha nyuma juhudi za mkoa kuhakikisha kwamba upatikanaji wa dawa na huduma bora kwa wananchi wanazikwamisha”,alisema Dkt Raphael.
Kwa upande wake kaimu mkurugenzi wa manispaa ya Shinyanga Sande Deogratius aliwataka watumishi wa serikali kuzingatia miiko na kanuni,misingi ya maelekezo ya kazi zao ikiwa ni pamoja na kufanya kazi kwa weledi kwani serikali inafanya juhudi kubwa za kuhakikisha kwamba inatoa huduma bora kwa wananchi .
Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga Justus Kamugisha alithibitisha kukamatwa kwa muuguzi huyu na kwamba bado wanaendelea kumhoji juu ya tukio hilo.
Na Kadama Malunde-Malunde1 blog
Social Plugin