ASKOFU MATHEW SHIJA AZIKWA HUKO KAHAMA,NI YULE MUASISI WA JIMBO KATOLIKI KAHAMA

Baadhi ya mapadri na viongozi wa dini walioshiriki katika misa ya maziko ya Askofu Mathew Shija
 

Mwasisi wa Jimbo Katoliki la Kahama mkoani Shinyanga Hayati Mhashamu Askofu Mathew Shija amezikwa leo katika Kanisa Kuu la Kiaskofu la Karoli Rwanga, mjini Kahama.

Akitoa salaamu kwa niaba ya maaskofu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), mhashamu askofu Ngalalekumtwa amesema askofu Shija alikuwa kiongozi wa kanisa aliyetoa mchango mkubwa wa kuwaunganisha maaskofu wenzake na kujenga umoja na mshikamano madhubuti katika mambo mbalimbali ya kitume na kwamba atakumbukwa daima na baraza hilo kwa mchango wake huo.


Amesema askofu Shija atakumbukwa kwa kutoa huduma za kitume na kiroho bila kujali tofauti za kidini na kiimani wakati wa uhai wake.

“Nikiwa Rais wa TEC nimepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha Baba Askofu mstaafu mhashamu Matheo Shija, Sisi maaskofu wa TEC tutamkukumbuka hayati askofu Shija kwa kufanya kazi kwa bidii na kujitahidi kujenga umoja na mshikamano ndani ya baraza kitu ambacho kilisaidia kuimarisha huduma za kitume za baraza letu"amesema mhashamu Ngalalekumtwa.

“Nakumbuka alipoteuliwa kuwa Askofu wa kwanza wa jimbo hili alikuwa mtu mzima wa miaka 60 ambao ni umri wa kustaafu lakini alifanya kazi kwa bidii na atakumbukwa kwa kufanikiwa kuasisi huduma ya kiroho kwa wafungwa wa gereza la Kahama bila kujali makundi ya kidini na kiimani”ameeleza mhashamu Ngalalekumtwa.


Akitoa salaam za rambirambi kwa Askofu wa Jimbo la Kahama mhashamu Ludovick Minde, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Magufuli amesema serikali imeshtushwa na taarifa za kifo cha Askofu Shija na kwamba serikali yake ipo pamoja na waumini na maaskofu wote wa kanisa katoliki katika kipindi hiki kigumu.


Kwa upande wake Balozi wa Vatican nchini Francisco Padia ameelezea kushtushwa na kifo cha askofu Shija na kutoa salaam za pole na Baraka kwa waumini na watu wote waliohudhuria mazishi hayo.

Askofu mstaafu Mathew Shija wa Jimbo Katoliki Kahama, Tanzania amefariki dunia hapo tarehe 9 Desemba 2015 na kuzikwa leo ndani ya kanisa la mtakatifu Karoli Rwanga na kuhudhuriwa na zaidi ya maaskofu 20 wa majimbo mbalimbali ya kanisa katoliki hapa nchini wakiongozwa na Rais wa TEC Ngalalekumtwa.



Askofu Shija alizaliwa huko Puge, Jimbo kuu la Tabora kunako tarehe 17 Aprili 1924. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, akapewa Daraja Takatifu la Upadre hapo tarehe 17 Januari 1954.


Tarehe 11 Novemba ,1983 Baba Mtakatifu Yohane Paulo II akaunda Jimbo Jipya la Kahama, Tanzania na kumteua Mheshimiwa Padre Mathayo Shija kuwa Askofu wa kwanza wa Jimbo Katoliki la Kahama na kuwekwa wakfu hapo tarehe 26 Februari 1984.


Baada ya kuitumikia Familia ya Mungu Jimbo Katoliki Kahama kwa ari na moyo mkuu, akang’atuka kutoka madarakani hapo tarehe 24 Aprili 2001.

Mhashamu Matthew Shija, ambaye alijiuzulu baada ya kufikia umri wa kupumzika ambao kwa mujibu wa Sheria za Kanisa Katoliki, ni miaka 75 .


Kufuatia hali hiyo baba Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili, akamteua Makamu wa Mkuu wa Shirika la Mapadre wa Maisha ya Kitume katika Kazi ya Roho Mtakatifu(ALCP/OSS), Padre Ludovick Joseph Minde, kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Kahama.

Marehemu Askofu mstaafu Mathayo Shija amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 91 tangu alipozaliwa.



Miaka 61 ya huduma kwa familia ya Mungu nchini Tanzania kama Padre na miaka 31 ya utume wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu Jimbo Katoliki Kahama, Tanzania.

Na Paul Kayanda -Malunde1 blog Kahama

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post