Askofu wa jimbo katoliki la Shinyanga mhashamu Liberatus Sangu (pichani)ameeleza kushangazwa na kusikitishwa na vitendo vya mataifa makubwa duniani kuhubiri amani duniani wakati wao ndiyo wana viwanda vikubwa vya kutengeneza silaha za kivita na kuuza ili watu waendelee kupigana matokeo yake kusababisha vifo,mateso na mahangaiko katika mataifa huku wahanga wakubwa wakiwa ni watoto,akina mama na wazee.
Akitoa mahubiri katika adhimisho la misa takatifu ya Krismasi leo iliyofanyika katika kanisa kuu la Mama Mwenye Huruma la Ngokolo mjini Shinyanga Askofu Sangu alisema wakati dunia inaadhimisha sikukuu ya Krismasi mataifa mengi hayana amani vita inaendelea na watu wanaishi katika dhiki kubwa kutokana na baadhi watu kuwa na uchu wa madaraka na fedha.
Askofu Sangu aliomba nchi zilizo katika vita ziombewe sana ili mwenyezi mungu aweze kuleta amani huku akieleza kusikitishwa na kushangazwa na mataifa yanayoshughulikia amani duniani kudai wanataka amani wakati ndiyo wenye viwanda vikubwa vya kutengeneza silaha za kivita.
“Tunasherekea sikukuu ya kuzaliwa Yesu Kristo wakati maeneo mengi duniani hakuna amani,mataifa makubwa yanayohubiri amani ndiyo wana viwanda vikubwa vya kutengeneza silaha, wanauza wapi? Ili upate soko la silaha,lazima utengeneze vita,watu wapigane,ili bidhaa itoke,lakini ndiyo hao wanaokaa mezani na kusema amani..amani”,alieleza Askofu Sangu.
Askofu Sangu alisema upo uwezekano mkubwa wa kuleta amani duniani lakini mataifa makubwa hajanuia kuleta amani kutokana na uchu wa madaraka,kutafuta biashara na fedha vyote hivyo vinasababisha watu kuishi maisha ya mateso na mahangaiko.
“Kutokana na uchu wa madaraka na fedha ,watu wanakufa,watoto,akina mama,wazee wanakufa kwa sababu ya ving’ang’anizi vya madaraka,tuwaombee wenzetu,mwenyezi mungu apate kuwajalia amani na utulivu ili sote kama familia ya watoto wa mungu tufike kule kristo ametutangulia”,aliongeza Askofu Sangu.
Akizungumzia kuhusu amani ya Tanzania wakati akitoa salamu za Krismasi,Askofu Sangu aliwataka wananchi kuwapuuza watu wanaosema nchi haina amani na kusisitiza kuwa Tanzania ni yenye amani na kuwataka watanzania kumwombea rais John Pombe Magufuli aliyeonesha nia ya kuwatumikia wananchi bila upendeleo ambaye ameonesha wazi wazi kuwa ana mtanguliza mwenyezi mungu.
“Kuna baadhi ya watu wanataka kutusadikisha kuwa Tanzania hakuna amani kwa nia zao wenyewe,labda wakilinganisha Tanzania na mbinguni ni sawa, kwa sababu mbinguni kuna utumilifu wake wote,lakini ukilinganisha Tanzania na mataifa mengine,ndugu zangu tuna amani ambayo tunapaswa kuilinda kwa nguvu zetu zote”,alieleza Sangu.
“Wapo wengi wangetamani tuchinjane hapa nchini,wa awivu,chuki na nchi yetu,na pengine wanaweza hata kutumia viongozi mbalimbali kupenyeza mambo yao ili tuchukiane sisi kwa sisi,tuwakemee watu wanaodharau hii amani iliyopo”,aliongeza askofu Sangu.
Alisema Tanzania hata bomu likilipuka watu wanakimbia kwenda kutazama,lakini kwa nchi zenye machafuko likilipuka bomu hakuna anayekwenda pale kwa kuhofia kifo,lakini watanzania ni kinyume na hiyo ni dalili tosha kuwa kuna amani.
Askofu Sangu aliwataka watanzania kusherehekea sikukuu kwa upendo hususani katika ngazi ya familia na kuhamasisha watu kuishi kwa kupendana na kuepuka vitendo vya kupeana ujumbe wa chuki na kujengeana chuki kwani ndiyo chanzo cha vurugu katika jamii na taifa kwa ujumla.
Katika hatua nyingine alisema siyo jambo zuri kwa watoto kwenda kwenye kumbi za starehe na kusisitiza kuwa familia yoyote iliyo bora haiwezi kumruhusu mtoto kwenda disko.
Na Kadama Malunde-Malunde1 blog
Social Plugin