Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinafanyia kazi uteuzi wa Katibu Mkuu wa chama hicho kufuatia aliyekuwa Katibu Mkuu wake, Dk. Willbrod Slaa kujivua wadhifa huo baada ya kujitoa kwenye siasa za vyama.
Pamoja na kutokuwa tayari kumtaja mrithi wa Dk. Slaa, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe anatarajiwa kuteua jina la mwananchama ambaye atashika wadhifa huo.
Katika majina yanayochomoza miongoni mwa wana-CHADEMA kushika mikoba hiyo ni jina la Waziri Mkuu mstaafu wa awamu ya tatu, Frederick Sumaye na aliyekuwa mgombea mwenza wa CHADEMA, akiungwa mkono na UKAWA, Duni Juma Haji maarufu kama "Babu Duni'.
Duru za kisiasa zinaeleza kuwa uamuzi wa hivi karibuni wa Frederick Sumaye kujiunga na CHADEMA ni moja katika mchakato mzima wa kumwezesha kuteuliwa kushika nafasi hiyo ya juu katika utendaji katika CHADEMA.
Chama hicho kinaona haja ya kumpa wadhifa huo Sumaye ili aendelee kuwepo katika medani za kisiasa na hivyo kumweka katika haiba nzuri ya kuendelea kuwa mpiga debe wa CHADEMA katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 na chaguzi zote ndogo zitakazojitokeza kufuatia rufani za wagombea ubunge wa CHADEMA waliokata rufaa kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika okroba 25, 2015.
Kwa upande wa Duni Juma Haji, ambaye awali alisemekana kuwa na mpango wa kurudi CUF ambako anadaiwa kuwa na kazi maalum, ameendelea kuwepo CHADEMA kimahesabu kwa matarajio kwamba endapo Seif Sharrif Hamad atafanikiwa kuwa Rais wa SMZ basi Babu Duni atafaa kuwa Katibu Mkuu wa CHADEMA ili kudumisha mahusiano kati ya CHADEMA na CUF.
Hili nalo limekaa katika mfumo ule ule wa mahesabu ya kisiasa kwani CHADEMA wanamwona Babu Duni kuwa ni mtaji wa uhusiano huo kati ya vyama hivyo vikuu vya upinzani nchini ambapo mtaji huo utwawezesha CHADEMA kuingia Ikulu ya Magogoni katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
Via>>Mpekuzi blog
Social Plugin