Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DC KAHAMA AIPINGA POLISI SAKATA LA WIZI WA MITIHANI,ADAI NI UVUMI TU WA KUHARIBU TASWIRA YA ELIMU KATIKA WILAYA YAKE


SERIKALI wilayani Kahama,imepinga madai ya baadhi ya walimu wa Sekondari kushikiliwa na polisi kwa kuhusika na kukutwa na majibu ya mtihani wa taifa wa kidato cha nne, kuwa ni uvumi uliolenga kuharibu taswira ya elimu ya wilayani humo.

Akiongea na waandishi wa Habari,Mkuu wa Wilaya ya Kahama,Vita Kawawa, alisema baada ya kuulizwa na waandishi wa Habari,alitumia vyombo vyake vya ulinzi na usalama vya wilaya na kubaini katika Halmashauri tatu zilizomo wilayani mwake hakuna tukio lolote la kuibiwa kwa mitihani ya Taifa ya Kidato cha nne.


Kauli hiyo ilikuja baada ya kuwepo kwa utata kwenye tukio hilo,ambalo kwa mujibu wa baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii vilimnukuu aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga,akidai polisi wilayani Kahama inawashikilia kwa uchunguzi walimu wawili kati ya 12 wa shule ya sekondari ya Anderlek Ridgers wanaodaiwa kukutwa na majibu ya mtihani wa somo la historia.

Kawawa alisema baada ya kupata taarifa hizo dhidi ya walimu wa shule hiyo alianza kufuatilia kwa makini tuhuma hiyo na kubaini kuwa ni uvumi wala hapakuwa na walimu waliosimamia mitihani kukutwa wameiba ama wanafunzi wahitimu kuingia katika vyumba vya mitihani wakiwa tayari majibu ya somo lolote katika wilaya ya Kahama.


“ Mimi kama mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Kahama, vyombo vyangu vya ulinzi na usalama niliviagiza kufuatilia kwa kina taarifa hizo na kubaini madai hayo ni uvumi,na kwakuwa yalikuwa na lengo la kuchafua taswira ya elimu nimeviagiza kumtambua “source”wa uvumi ili sheria ichukue mkondo dhidi yake,”alisema Kawawa.

Alisema taarifa hizo zilizotolewa katika baadhi ya vyombo vya habari kupitia Magazeti ya tarehe 5/12/ 2015 yalinukuliwa yakiandika kuwa Wawili wamefikishwa Mahakamani kwa kosa la kukamatwa na mitihani ya kidato cha nne jambo ambalo siyo la kweli na kuongeza kuwa Mkuu huyo wa Wilaya alisema kuwa Serikali inafanya jitihada za kuwasaka waliovumisha taarifa hizo.


Kawawa aliwataka Wananchi wapuuze uvumi uliotolewa na vyombo mbalimbali vya habari kuhusiana na tukio hilo kwani ni la upotoshaji likiwa na lengo la kuichafua Serikali pamoja na Watendaji wake na kuongeza kuwa hakuna tukio kama hilo lililoripotiwa katika ofisi yeye akiwa kama Mwenyekiti wa Kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya.

“Ndugu Waandishi wa Habari taarifa hizo milizozisikia au kuzisoma katika vyombo vya habari kuhusu tuhuma za Walimu wawili walidaiwa kufikishwa Mahakamani sii za kweli na ninatoa onyo kali kwa wote waliohusika katika kusambaza taarifa hizo kwani zilikuwa na lengo la kuichafua Serikali na hivyo Sheria itafuata Mkondo wake”, Alisema Vita Kawawa.


Kwa upande wake,Ofisa elimu ya Sekondari katika Halmashauri ya Mji wa Kahama,Anastazia Manumbu,ambapo ndipo ilipo sekondari ambayo walimu wake walidaiwa kurushiwa majibu hayo kutoka mkoani Kagera,alisema katika mitihani ya taifa ya kidato cha pili na cha nne iliyomalizika Novemba 27 mwaka huu, hakukuwa na tukio lolote la walimu ama wanafunzi kukamatwa na majibu ya mitihani hiyo.


Manumbu alisema kamati yake ya mitihani ya taifa ya kidato cha pili na cha nne ilijiridhisha wasimamizi wa mitihani walitekeleza majukumu yao kwa umakini wa hali ya juu kwa kufuata sheria na kanuni zote za baraza la taifa la mitihani na kumaliza kwa amani na hakuna msimamizi aliyehojiwa ama kushikiliwa na Polisi,hata wanaodaiwa kukamatwa hawakuwa wasimamizi wa mitihani.



Nae Mkurugenzi wa shule ya sekondari ya Anderleck Ridges , Alexander Kazimil, alipoulizwa alisema wanafunzi wake hawana uhusiano na kuibiwa kwa mitihani hiyo,na kukamatwa kwa walimu wake ilikuwa ni mpango wa kuichafua shule yake ili kuharibu sifa iliyojijengea ndani na nje ya nchi,kwa kuwatumia mtihani wa historia kwa njia ya simu zao za mikononi,walimu ambao hawakuwa wasimamizi ama kuhusika kusogea kwenye kituo cha kufanyia mitihani.

“Si mwalimu ama mwanafunzi anayehusika,bali kilichohusika ni pesa iliyotumika kuandaa mpango wa kutengeneza mazingira ya kuingamiza taasisi ya Anderlek,lakini mtu huyo atambue wakati mwingine pesa hukwama na ndipo atakapoumbuka,ninachoomba Baraza la Mitihani lisahihishe mtihani wa somo tunalotuhumiwa kwa umakini mkubwa,ili kubaini ukweli wa tuhuma hizo,”alisema Kazimil.

Hata hivyo kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga Justus Kamugisha alisema swala hilo bado wanaendelea kulifanyia uchunguzi kwa kukusanya takwimu na wanataraji kulitolea ufafanuzi katika vyombo vya habari mapema wiki hii.




Hivi karibuni Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga lilidai kuwachunguza walimu wawili wa sekondari hiyo baada ya kupatiwa taarifa kuwa walitumiwa majibu ya somo la historia kwa njia ya simu na mtu mmoja kutoka mkoani Kagera,na kuwachunguza walimu 12 kabla ya kuwashikilia wawili kwa uchunguzi zaidi.

Na Paul Kayanda na Ali Lityawi-Kahama

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com