MBUNGE wa Ubungo, Saed Kubenea (Chadema), nusura azichape kavu kavu na Mkuu wa Wilaya ya Kinodnoni, Paul Makonda baada ya kutokea kutoelewana.
Kutokana na hali hiyo Makonda aliwaagiza askari wa Jeshi la Polisi kumtia mbaroni Kubenea kwa kile kilichoelezwa kuwa mbunge huyo ameshindwa kutii agizo la mkuu huyo wa wilaya.
Tukio hilo lilitokea jana, jijini Dar es Salaam, baada ya viongozi hao kukutana katika mgomo wa wafanyakazi wa Kiwanda cha nguo cha Tooku Tanzania, ambapo Kubenea alikuwa wa kwanza kufika kwa ajili ya kutatua mgogoro wa wafanyakazi wa kiwanda hicho.
Katika mgomo huo Kubenea, alisikiliza kero za wafanyakazi ambao walikuwa wakivutana na menejimenti ya kiwanda hicho na baada ya makubaliano yaliyohusisha pande mbili walikubali kuendelea na kazi.
Hata hivyo wakati mbunge huyo pamoja na viongozi wa kiwanda hicho wakiwa katikati ya mazungumzo Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda, aliwasili katika eneo hilo la kiwanda kilichopo ndani ya Mamkala ya Uwekezaji EPZ Mabibo External.
Baada ya kufika katika eneo hilo, Makonda hakutaka kuhoji kuhusu kilichoendelea kuhusu mgomo huo wa wafanyakazi na kutaka kuanza upya kusikiliza malalamiko ya wafanyakazi licha ya Kubenea kuupatia ufumbuzi kwa mazungumzo yaliyohusisha pande zote.
Kutokana na hatua hiyo, Kubenea hakupinga hatua hiyo ingawa Makonda alipomaliza kuzungumza na wafanyakazi wa kiwanda hicho, alifunga mkutano bila kuruhusu hoja yoyote kutoka kwa mbunge huyo.
Hali hiyo ilimfanya Kubenea kuhoji sababu ya kutopewa nafasi ya kuzungumza wakati ndiye alikuwa wa kwanza kufika katika eneo la tukio tangu saa nne asubuhi na kulimaliza suala hilo.
Pamoja na hali hiyo Makonda, alipinga hoja ya Kubenea kuzungumza na wafanyakazi hao na kusema kwamba tayari amekwisha kufunga mkutano, hivyo haruhusiwi mtu mwingine kuzungumza kwa kuwa ndiye alikuwa mzungumzaji wa mwisho na tayari alikuwa ameshafunga.
Hatua hiyo ilizua mabishano makali baina ya Kubenea na Makonda kwa kila mmoja kusimamia kile anachokiamini.
Wakati hayo yakiendelea, Kubenea aliendelea kuwasihi wafanyakazi hao watulie, lakini Makonda akasisitiza hatozungumza hali iliyosababisha polisi waliokuwapo katika eneo hilo na baadhi ya viongozi wa kiwanda kuingilia kati kusuluhisha mzozo huo.
“Huwezi kufunga mkutano nisiongee na wafanyakazi ambao ni wapiga kura wangu, nimekuja hapa tangu asubuhi nimepambana hadi tukafikia hapa na niliwaahidi nikitoka kwenye kikao cha utawala nitawapa mrejesho (yaliyojiri).
“Inakuwaje wewe umekuja sasa hivi unazungumza na kufunga mkutano kwa ubabe?,” alihoji Kubenea huku Makonda akiendelea kusimamia msimamo wake kwamba tayari amefunga mkutano.
“…mimi hawa wamenipigia kura, wewe umepata kura ngapi, huwezi kunifanya lolote wewe,” alisema Kubenea.
Baada ya mabishano hayo, Makonda aliamuru Kubenea akamatwe pamoja na kuamuru mwandishi wa Kituo cha Televisheni cha Star TV kunyang’anywa kamera yake.
Polisi walimtaka Kubenea kupanda kwenye gari lao la polisi (Defender) lakini kukatokea mabishano makali, kwani Kubenea alipinga kupanda gari lao umuazi waliokukubali na hatimaye askari wawili wenye silaha na mmoja ambaye hakuwa na silaha waliingia kwenye gari la mbunge huyo hadi Kituo cha Polisi cha Magomeni.
Wanasheria wazungumza
TUNDU LISSU
Mwanasehria Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, alisema mkuu wa wilaya ana mamlaka ya kuamuru mtu aliyefanyakosa mahali ambako hakuna polisi akamatwe.
“Kama kuna polisi kwenye eneo la kosa hayo mamlaka hawezi kuwa nayo, na kama akitoa amri hiyo atakuwa anawajibika kutoa maelezo na sababu za kumkamata mtu huyo kwa hakimu wa wilaya.
“Alichokifanya DC wa Kinondoni ni uvunjaji wa sheria na tutamshughulikia hadi ataikimbia hiyo wilaya,” alisema Lissu.
KIBATALA
Akizungumzia kuhusu mamlaka ya mkuu wa wilaya kutoa amri ya kukamatwa mbunge, mwanasheria Peter Kibatala alisema amefurahi kutokea kwa kesi hiyo na anaomba suala hilo kwenda mahakamani kama shtaka la jinai.
Alisema kesi hiyo itasaidia kuhoji mamlaka ya mkuu wa wilaya na namna ambavyo anayatekeleza.
“Vyovyote iwavyo lazima tuhakikishe tunawasilisha malalamiko kwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ili kupata uamuzi wa nini hasa mipaka kati ya serikali na maafisa wake na wabunge hasa wa upinzani,” alisema Kibatala.
FREDERICK KIHWELO
Kwa upande wake mwanasheria wa mbunge huyo, Frederick Kihwelo alisema jambo la msingi katika suala hilo ni kuhakikisha cheo hicho kinaondolewa ili kiweze kuwaacha polisi wafanye kazi zao kwa uhuru.
“Inasikitisha kuona mkuu wa wilaya ni kada wa CCM, mjumbe wa siasa wa wilaya wa CCM na ndiye mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wa wilaya hivyo ni bosi wa OCD na ofisa usalama wa wilaya,” alisema.
Aliwataka wale waliopewa mamlaka hayo kuhakikisha wanatumia mamlaka hayo kwa busara badala ya kutumia nguvu na jeuri.
Via>>Mtanzania
Social Plugin