Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

JINSI MOTO WA RAIS MAGUFULI ULIVYOICHOMA TANESCO..TIMUA TIMUA YAANZA



MOTO wa utendaji kazi wa Rais Dk.John Magufuli umetua ndani ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) baada ya shirika hilo kuwafukuza kazi mameneja, wahandisi na wahasibu kutokana na ubadhirifu mkubwa.


Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Felchesmi Mramba amesema uamuzi huo umechukuliwa kupambana na vitendo vya wizi na ubadhirifu vinavyofanywa na wafanyakazi wasiokuwa waadilifu.

“Tumechukua uamuzi mgumu wa kuwafukuza maofisa wetu kutokana na kujihusisha na vitendo mbalimbali.

“Huu ni mwanzo tu tumedhamiria kupambana na wafanyakazi wasiokuwa waadilifu ndani ya shirika,”alisema Mramba alipozungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana.

Alisema maofisa saba wamefukuzwa kazi katika mikoa ya Dodoma (Kondoa Kaskazini), Kagera, Shinyanga, Katavi na Mkoa wa Tanesco wa Ilala.



Kati ya maofisa hao waandamizi kuna waliofikishwa mahakamani mkoani Kagera wiki iliyopita kujibu tuhuma zinazowakabili, alisema.

“Kwa mfano, wale maofisa wa mkoani Kagera wiki iliyopita walifikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.

“Katika kukabiliana na tatizo hili, tupo kwenye maandalizi ya kutoa namba maalumu za simu kwa wateja.

“Namba hizi hazitalipiwa gharama yoyote ila zitatumika kutoa taarifa ya vitendo vya wafanyakazi ili hatua zichukuliwe,”alisema Mramba.

Alisema shirika limeanza kuwachuklia hatua wafanyakazi wanaobainika kujihusisha na vitendo mbalimbali ambavyo ni kero kwa wateja.

Vitendo hivyo ni pamoja na lugha mbaya, wateja kudaiwa rushwa na kucheleweshwa huduma, alisema.



WATEJA



Kuhusu kudhibiti wizi wa umeme, Mramba alisema shirika limetoa siku saba kwa wateja wanaojua mita zao zimechezewa kujisalimisha wenyewe kwa mmeneja wa mikoa.

Alisema baada ya siku hizo utafanyika msako wa wezi na wote watakaokamatwa watawekwa hadharani na baadaye kushtakiwa.

“Ndani ya siku hizi hatatuchukua hatua zozote kwa mteja, baada ya kupita muda huo hatua kali zitachukuliwa kwa kufuata sheria ikiwamo kunadi mali zao kufidia deni kama hana uwezo wa kulipa.

“Nawaomba wateja wetu, kipindi hiki ambacho tunaendelea kuboresha miundombinu yetu ya uzalishaji wawe wavumilivu kwa usumbufu unaoweza kujitokeza.

“Naamini tutajitahidi kadri ya uwezo wetu kurekebisha kasoro zinazoweza kurekebishwa katika miundombinu ya sasa kupunguza usumbufu utakaojitokeza,”alisema.

Alisema kuanzia Januari mwakani umeme unaotokana na gesi nchini utafikia megawati 700 ikiwa ni asilimia 70 ya umeme wote kwenye Gridi ya Taifa.

“Haya ni mapinduzi makubwa kuwahi kutokea katika uzalishaji wa umeme kutokana na ukweli kuwa miaka mingi tulikuwa tunatumia vyanzo vya maji kwa zaidi ya asilimia 70 hivi,” alisema Mramba.



Alisema tangu Septemba 17 mwaka huu gesi kutoka Mtwara ilipoanza kutumika uzalishaji umeme kwa kutumia gesi umeongezeka kutoka megawati 260 za zamani hadi megawati 540.

Mramba alisema hilo ni ongezeko la megawati 300 kitendo ambacho kinachangia kuboresha hali ya upatikanaji wa umeme.

Alisema shirika linatarajia kuongeza umeme wa megawati 130 kutoka vyanzo vya gesi kati ya sasa na Januari mwakani na kufanya umeme wa gesi kufikia megawati 700, kiasi ambacho ni asilimia 70 ya umeme wote kwenye Gridi ya Taifa.

“Nawaambia ndugu zangu haya nimapinduzi makubwa, miaka mingi vyanzo vya maji vimekuwa mkombozi wa taifa hili.

“Lakini ulipokuwa ukitokea ukame kila mmoja wetu anatambua athari zilizokuwa zikijitokeza,”alisema.

Alisema mkandarasi wa mradi wa pili wa Kinyerezi II wa megawati 240 kutoka Japan anatarajiwa kuanza kazi mwezi huu au ujao.



NGUZO



Akizungumzia ununuzi wa nguzo nje ya nchi, Mramba alisema kuna wasambazaji kadhaa wa nguzo kutoka ndani na nje ya nchi na hupatikana kulingana na sheria ya ununuzi na vigezo vya ubora.

“Yamekuwapo malalamiko mengi ya ununuzi wa nguzo za umeme.

“Naomba niwahakikishie kuwa wapo wasambazaji ambao tunaingia nao mikataba kwa kuangalia vigezo vingi vikiwamo vya ubora na Sheria ya Ununuzi…hakuna kitu ambacho kinakwenda kinyume cha sheria.



KAZI YA MAGUFULI

Rais Magufuli hivi sasa amekuwa gumzo ndani na nje ya Afrika kutokana na utendaji kazi wake.

Wachambuzi na wafuatiliaji wa mambo wamekuwa wakielezea staili yake ya utekelezaji wa majukumu ya urais kuwa itanyoosha mambo mengi yaliyokuwa yamepinda.

Ziara ya kushtukiza ya Rais Magufuli katika Wizara ya Fedha ilibadili mwenendo wa siku nyingi wa watumishi na maofisa ambao baadhi yao wamekuwa wakisikika wakieleza kuwa sasa wanawajibika kuwapo sehemu zao za kazi kwa muda wote tofauti na mwenendo wa awali.

Rais Magufuli pia alitangaza kufuta ziara zisizo za lazima za watumishi na maofisa wa Serikali nje ya nchi.

Vilevile alipiga marufuku semina, makongamano, warsha na mikutano ya wajumbe wa bodi wa mashirika na taasisi za umma kufanyikia kwenye kumbi za hoteli za kifahari na badala yake ifanyikie kwenye kumbi za mashirika au taasisi husika.

Hadi sasa hatua zinazochukuliwa na Rais Magufuli za kuleta mabadiliko ya mfumo wa utendaji kazi serikalini zimeokoa zaidi ya Sh trilioni moja.

Tayari mabingwa wa uchumi wameeleza kuwa zipo dalili njema kwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 kuipeleka Tanzania katika nchi ya uchumi wa kati.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa naye alifanya ziara ya kushtukiza Mamlaka ya Bandari (TPA) Novemba 27 ambako aligundua udanganyifu mkubwa katika ulipaji kodi.

Aliamuru kusimamishwa wafanyakazi watano wa TRA na muda mfupi baadaye Rais Magufuli alimsimamisha kazi Kamishna Mkuu wa TRA, Rished Bade.

Wiki iliyopita, maofisa wa TRA wasiopungua wanane walifikishwa mahakamani jijini Dar es Salaam wakikabiliwa na mashitaka ya kuliingizia taifa hasara ya mamilioni ya fedha kutokana na kodi ambayo haikulipwa. 
 Chanzo-Mtanzania

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com