KAULI YA "TUMBUA MAJIPU" YAMPONZA BINTI MTUMIAJI WA FACEBOOK, AKAMATWA NA POLISI


Mtu mmoja anashikiliwa na jeshi la polisi mkoani Mbeya kwa tuhuma za matumizi mabaya ya mtandao wa Face book.


Mtuhumiwa huyo aliyefahamika kwa jina la Carolne Kajela, alikamatwa jioni ya desemba 12, mwaka huu eneo la Uyole Jijini hapa, baada ya kuandika katika ukurasa wake wa Facebook kupitia kundi la Kwinyara Let’s talk kuwa, mmiliki wa mabasi ya Rungwe Express anaingiza mabasi hayo kupitia taasisi ya dini.


“Mtumbua majipu atumbue na hili.. mmiliki wa mabasi ya RUNGWE EXPRESS anapitisha mabasi kupitia taasisi moja ya kidin imbombo... jilipo,” unasomeka ujumbe huo, ambao mpaka anakamatwa ulikuwa umependwa na watu 35 na kuchangiwa maoni na watu 120


Taarifa kutoka ndani ya jeshi la polisi zinasema baada ya mtuhumiwa huyo kukamatwa na kuhojiwa, amekiri kosa na kuomba asamehewe kwani shetani alimzidi.


Mmiliki wa mabasi hayo Yohana Sonelo, alipohojiwa amekiri kampuni yake kupeleka mashitaka polisi na kwamba wanahitaji athibitishe alichokiandika mtandaoni, lasivyo sheria ya makosa ya mtandao namba 14 ya mwaka 2015 ambayo ilianza kutumika Septemba Mosi mwaka huu ifuate mkondo wake.


Kamanda wa polisi mkoani Mbeya, Ahmed Msangi, amethibitisha kumkamata mtuhumiwa huyo na kwamba taratibu za upelelezi zinaendelea kisha watapeleka jalada kwa mwanasheria wa serikali ili mtuhumiwa afunguliwe mashitaka na afikishwe mahakamani.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post