Aliyekua mgombea Urais anayeungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa, ameendelea kudai ndiye mshindi kwenye Uchaguzi Mkuu uliopita na dunia inajua.
Katika taarifa aliyoitoa jana kwa vyombo vya habari kupitia msemaji wake, Aboubakary Liongo, Lowassa alisema ushindi wake uliporwa na kupewa mtu mwingine lakini amewataka Watanzania wasikate tamaa.
Lowassa pia aliwashukuru Watanzania kwa kumpa kura nyingi wakati wa uchaguzi huo, kura ambazo alidai kuwa zilimfanya kuongoza dhidi ya wagombea wengine.
Hata hivyo, katika uchaguzi huo wa Oktoba 25, Rais John Magufuli ndiye aliyeshinda kwa kupata kura 8,882,935 (sawa na asilimia 58.46) na Lowassa kura 6,072,848 (sawa na asilimia 39.97) ya kura zote.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Damian Lubuva alimtangaza Dk. Magufuli kuwa Rais mteule siku nne baadaye na aliapishwa Novemba 5, mwaka huu.
Liongo alisema Lowassa alitoa shukrani hizo juzi jioni katika mikutano ya hadhara wa kumnadi mgombea ubunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema kwenye kata za Mkonoo na Nodisaito.
“Nawashukuru sana Watanzania kwa kanipa kura nyingi kabisa. Tulishinda, dunia nzima inajua na wao wanajua, Watanzania mmeonyesha imani kubwa kwangu,” amekaririwa Lowassa.
“Nawashukuru sana Watanzania kwa uvumilivu wenu baada ya kushuhudia ushindi wenu ukiporwa… mlitaka wakati ule nitoe tamko muingie barabarani kudai ushindi wenu.
“Lakini nawapenda, Watanzania siko tayari kuona mnapoteza maisha,” imesema taarifa hiyo ikimkariri Lowassa.
Aliwaomba wananchi wa Arusha kumchagua Lema katika Uchaguzi wa jimbo hilo kesho ili kuliletea maendeleo Jiji la Arusha ambalo linaongozwa na Ukawa.
Na Mary Geofrey -NIPASHE
Social Plugin