Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.Dr John Pombe Magufuli ametangaza Baraza la Mawaziri ambalo litafanya kazi katika serikali hii ya awamu ya tano kwa kipindi cha miaka 5.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dr es salaam Rais Dr. Magufuli ametangaza baraza la wizara 18 na katika wizara hizi kutakuwa na mawaziri 19 na nyingine zitakuwa hazina manaibu waziri kabisa wote watatakiwa kuanza kazi mara moja bila kusubiri semina elekezi kama ilipozoeleka hapo awali.
“Nimeteua baraza dogo la mawaziri kwa lengo la kuepuka gharama za matumizi yao pamoja na watendaji wengine na fedha ambazo zilikuwa zimeandaliwa na ofisi ya utumishi kiasi cha shilingi bilioni mbili na zaidi zitatumika katika shughuli nyingine muhimu kama vile kutengeneza madawati au eneo jingine muhimu zaidi.”
Aidha Dr Magufuli amewataka Mawaziri waliochaguliwa wakawatumikie Watanzania kwa yale waliyoahidi katika kipindi cha kampeni bila kubagua vyama vyao,dini,ukanda,tabaka na ndio maana kauli mbiu yetu inasisitiza kwamba “Hapa ni Kazi tuu”
Kwa upande mwingine Rais Dr. Magufuli ametamka wazi kwamba hakutakua na sherehe za kuwapongeza mawaziri hao na kama wanataka sherehe wajiandae pia kufanya sherehe siku ya kufukuzwa kazi.
“Nilipomteua waziri Mkuu alijielekeza moja kwa moja kwenye kufuatilia makontena na Makamu wa Rais akajielekeza kwenye Mazingira sasa na hawa wanatakiwa kujielekeza kwenye wizara zao bila kupoteza muda”alisisitiza Rais.
Baraza hili limechelewa kutangazwa kwa takribani mwezi mzima tangu alipoapishwa Dr Magufuli na hata hivyo wizara 4 bado hazijapatiwa Mawaziri ikiwemo Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Ujenzi uchukuzi na mawasiliano, Wizara ya Fedha na mipango na Wizara ya Sayansi Teknolojia,Elimu na Ufundi.
Via>>EATV
Social Plugin