Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi limewakamata na linawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kumshambulia kwa kumpiga na kumjeruhi Jeneroza Roba (60) Mkazi wa Mtaa wa Nsemlwa Mjini Mpanda baada ya kumtuhumu kuwa ni mchawi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi Dhahiri Kidavashari amesema tukio hilo limetokea juzi saa tano asubuhi katika mtaa wa Mji wa Zamani mjini hapo.
Kidavashari amewataja waliokamatwa na Polisi kuwa ni Ashura Msaguzi (30) Mkazi wa Mji wa Zamani ambae ni mtumishi wa chuo cha maendeleo ya jamii cha Msaginya Mkoani Katavi na Aisha Sungura (28) Mkazi wa mtaa wa mji wa Zamani.
Akielezea kuhusu tukio hilo amesema siku ya tukio Jeneroza alikuwa akipita kwenye mtaa wa mji wa Zamani akiwa anaelekea nyumbani kwake katika Mtaa wa Nsemlwa.
"Ndipo mtuhumiwa Ashura alipomwona Jeneroza na kuanza kupandisha mashetani huku akiwa anamtaja Jeneroza kuwa ndiye aliyemloga,...kitendo hicho cha kupandisha mashetani kilimshawishi Aisha kuungana na Ashura na kisha walianza kumshambulia kwa kumpiga Jeneroza na kisha walimvua nguo na kumwingiza ndani ya nyumba hiyo ",anasimulia Kamanda wa polisi.
Alisema kitendo hicho kiliwakasirisha watu walioshuhudia hali ambayo iliwafanya wananchi waanze kuishambulia kwa mawe nyumba hiyo kwa lengo la kumwokoa Jeneroza ambaye alikuwa amefungiwa ndani ya nyumba ya wazazi wake na Ashura.
Kufuatia kitendo hicho mwenyekiti wa Mtaa huo Magreth John alifika eneo la tukio kisha kutoa taarifa kwa jeshi la Polisi waliofika kisha kuwatawanya wananchi na kukamata watuhumiwa ambao mpaka sasa wanashikiliwa.
Na Walter Mguluchuma-Malunde1 blog Katavi
Social Plugin