Kaburi la marehemu |
Mwanamke aliyezungushiwa duara jekundu ndiye anayedaiwa kumuua mumewe na kumfukia.
NI simulizi ya kushangaza kufuatia Archard Frederick (41), kudaiwa kupigwa na kitu kizito kichwani hadi kufariki dunia na mkewe, chanzo kikitajwa kuwa ni wivu wa kimapenzi.
Tukio hilo lilijiri Desemba 11, mwaka huu Kijiji cha Irogelo, Kitongoji cha Buhesi, Kamachumu, Muleba, Kagera.
Mwenyekiti wa kijiji hicho, Prudence Rutaihwa alisema kabla ya Archard hajafariki dunia aligombana na mkewe.
Alisema marehemu alipotea ghafla jioni ya Ijumaa ya Desemba 11, mwaka huu saa 12 jioni.
“Jumamosi asubuhi wafanyakazi wenzake wa ujenzi walimpitia kwake ili waende kibaruani wakakuta mlango umefungwa. Walipompigia simu hakupatikana hewani, wakaondoka.
Alisema wenzake hao walijua watoto walikwenda machungani na mkewe alikwenda shamba lakini baada kutopatikana hewani, kaka wa marehemu, Projest Fredrick alipewa taarifa na kuanza kuwa na wasiwasi.
Kabuli alilozikwa marehemu huyo.
“Jioni ya Jumamosi, kaka wa marehemu alipokea simu kutoka kwa kaka yao mwingine aishiye Kisiwa cha Bumbire aitwaye Reontin Fredrick na kumuuliza kwa Segere kuna nini? Segere ni jina maarufu la marehemu.
“Reontin alimwambia Projest kuwa amepigiwa simu na mke wa Archard kuwa aende nyumbani kwake kuna matatizo,” alisema mwenyekiti huyo.
Habari zaidi zinasema kuwa Jumapili saa 8 mchana, mwenyekiti alimwandikia barua Reontin kumtaka aende nyumbani kwa wazazi wa mke wa marehemu kwa sababu mwanamke huyo aliondoka na watoto wote.
Reonton alipofika huko, alikutana na baba wa mke wa marehemu ambaye alimwambia kuwa binti yake alikunywa sumu lakini anamwomba Mungu apone.
“Alipoambiwa hivyo, Reonton aliamua kwenda Kituo cha Polisi Kamachumu kutoa taarifa na siku hiyohiyo usiku, majirani na Reonton walikwenda kulala kwa marehemu ili kulinda mifugo yake.
“Wakati wakikagua mazingira walikuta nguo nyingi zimetumbukizwa kwenye tundu la choo zikiwemo za watoto na za mke wa marehemu.
“Kwa vile ilikuwa usiku hawakuweza kuona vizuri, asubuhi ya Jumatatu walitaka kupiga ngoma ili waanze msako wa kumtafuta Archard lakini waliamua waende tena kuziangalia zile nguo.
“Wakiwa wanakwenda wakaona majani ya migomba yakiwa yamefunikwa vizuri na chandarua kilichochanika kisha juu yake yakawekwa majani ya maharage yakiwa yamenyooka.
“Tukio hilo lilitushtua wengi, tukaamua kufunua yale majani na kukuta mwili wa marehemu ukiwa na jeraha kubwa kichwani.
“Tulitoa taarifa polisi. Wakawahoji watoto wa marehemu ambapo walisema siku ya tukio baba yao alirudi nyumbani usiku wa saa mbili lakini mama yao hakuwepo hadi walipokwenda kulala.
“Walisema mama yao alirudi muda usiojulikana, wakasikia wanagombana na baba yao. Baada ya muda walisikia sauti moja ya baba yao akisema kwa lugha ya Kihaya ‘yooo’, akionesha mshangao. Hakusikika tena, wakajua amelala,” alisema mwenyekiti huyo.
Social Plugin