Moto mkubwa unaodaiwa kusababishwa na hitilafu ya Jenereta umeteketeza kliniki ya afya ya mapenzi kanda ya ziwa, iliyopo nyuma ya jengo la chama kikuu cha ushirika Nyanza jijini Mwanza huku baadhi ya wakazi wa jiji hilo wakililalamikia jeshi la zimamoto na uokoaji kutokana na kuchelewa kufika katika eneo la tukio.
Tukio la moto huo kwenye kliniki hiyo iliyopo jirani na benki kuu ya Tanzania tawi la Mwanza pamoja na benki ya NMB tawi la Kenyatta, limetokea majira ya saa nane mchana, muda mfupi baada ya kukatika kwa umeme wa Tanesco.
Watu walioshuhudia moto huo wanasema licha ya askari wa zimamoto kufanikiwa kuzima moto huo, changamoto kubwa iliyojitokeza ni vifaa duni na kuchelewa kufika eneo la tukio kwa wakati.
Afisa wa shughuli za jeshi la zimamoto na uokoaji Mwanza, mkaguzi msaidizi Simion Raphael anasema chanzo cha moto huo bado hakijajulikana, hata hivyo amejibu malalamiko yaliyoelekezwa kwa jeshi hilo na baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo.
Via>>ITV
Social Plugin