Baada ya kutaja Baraza la Mawaziri lenye sura mpya nyingi juzi ikiwa moja ya hatua katika ukamilishaji wa safu za uongozi wa serikali ya awamu ya tano, Rais John Magufuli anataraji kuondoa Wakuu wengi wa Mikoa na Wilaya kutokana na kukosa sifa, taarifa za uhakika zinasema.
Mbali na wawakilishi wa Rais hao katika ngazi ya Mkoa na Wilaya, panga kubwa litawakumba wakurugenzi wa Taasisi na Mashirika ya Umma nchini.
Taarifa kutoka ndani ya serikali zinaeleza kuwa Rais Magufuli ameshaitisha mafaili ya kumbukumbu za wasifu wa viongozi hao ili kujiridhisha na sifa zao.
Chanzo cha habari kutoka serikalini kimeidokeza Nipashe kuwa taasisi na mashirika ambayo yapo katika hatari ya kukubwa na fagio la Rais Magufuli ni pamoja na Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Taarifa zilieleza kuwa Rais Magufuli atachukua hatua hiyo kwa lengo la kuteua watendaji wapya ambao wataendana na kasi ya serikali ya awamu ya tano inayotekeleza kauli mbiu ya ‘Hapa Kazi Tu’.
“Unajua ma RC na ma DC wakati wa serikali ya awamu ya nne baadhi walipewa nafasi hizo kwa huruma ya kukosa ubunge ndiyo sababu baadhi yao wanashindwa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi,” kilisema chanzo hicho.
Fagio hilo litawahusisha pia watendaji ambao wakati wa serikali ya awamu ya nne walivurunda katika sehemu zao za kazi na kilichofanyika ni kuwahamisha na kupangiwa maeneo mengi.
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, hakuweza kulitolea ufafanuzi wa kina suala hilo alipoulizwa na Nipashe jana, akisema kuwa ni taarifa ngeni kwake.
Wakati wa serikali ya awamu ya nne ya Rais Jakaya Kikwete uteuzi wa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya ulikuwa ukipokelewa kwa hisia tofauti na wasomi na wanasiasa.
Wengi walidai hiyo imekuwa kama kichaka cha kuwahifadhi makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) waliobwagwa kwenye kura za maoni ndani ya chama hicho .
Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa kwanza ni Wakuu wa Ulinzi na Usalama katika maeneo yao (Wilaya na Mkoa) kwa maana kwamba wanamwakilisha Rais katika masuala yote ya Ulinzi na Usalama.
Aidha, wakuu hao ni wasimamizi wa shughuli za Maendeleo yote katika maeneo yao na wanawajibika kufuatilia utekelezaji wa miradi ili iweze kukamilika kwa muda na kwa kiwango kinachotakiwa.
Wakuu wa Mikoa/Wilaya ni wafuatiliaji na wasimamizi wa utekelezaji wa Sera mbali mbali za Serikali katika maeneo yao.
CHANZO: NIPASHE
Social Plugin