Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

VIONGOZI WA CHADEMA NA CCM WATWANGANA NGUMI




Zogo kubwa liliibuka katika kikao cha kuwachagua Meya na Naibu Meya wa Manispaa ya Dodoma jana. Zogo hilo lilisababisha viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuzichapa kavukavu.


Hali hiyo ilitokea wakati wa kuapisha madiwani 56 na kufanya uchaguzi katika Viwanja vya Ukumbi wa Manispaa hiyo mjini Dodoma, ilisababishwa na lugha za vijembe na kashfa kati ya vyama hivyo viwili.


Vurugu hizo zilizodumu kwa takribani dakika 20 ziliwakutanisha ana kwa ana Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Dodoma, Aifraim Kolimba (CCM) na Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Dodoma, Vicent Emmanuel ambao walikunjana.


Viongozi hao walikunjana kwa dakika kadhaa kabla ya mgambo wa Manispaa kuwatenganisha na kuwatuliza.

Pamoja na mgambo hao kurejesha hali ya utulivu, makada hao waliendelea kurushiana matusi ya nguoni huku kila mmoja akikashifu chama cha mwenzake.


Tukio hilo lilikoma mara baada ya Diwani wa Kata ya Kizota (Chadema), Jamal Yaled alipowataka makada na viongozi wa chama chake kutulia. “Jamani wala msipigane, hawa tutawanyoosha katika Baraza nawaomba mtulie,” alieleza Yaled.


Kuwasili kwa askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia, FFU, kulifanya vurugu iliyokuwepo awali kutulia na shughuli za uchaguzi kuendelea.

Katika uchaguzi huo, madiwani 48 kati ya 56 walimpitisha Japhary Mwanyemba kuwa Meya wa Manispaa hiyo kwa asilimia 82, huku Naibu Meya akichaguliwa Jumanne Ngede.


Akitangaza matokeo hayo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Clemence Mkusa alisema, “Namtangaza kwenu Jumanne Ngede kuwa Naibu Meya wa Manispaa ya Dodoma kwa kura 48 kwa asilimia 82 kama za Mwanyemba."


Akizungumza baada ya kuchaguliwa, Mwanyemba aliwataka madiwani hao kuvunja makundi kwa kuhakikisha wanatetea matatizo ya wananchi kwa kuwaletea maendeleo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com