Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WALIMU WAKAMATWA NA MITIHANI YA KIDATO CHA NNE SHINYANGA

Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga Justus Kamugisha


Walimu wawili wa shule ya sekondari ya Anderlek Redger, iliyoko Kahama mkoani Shinyanga, wanachunguzwa na Jeshi la Polisi kufuatia tuhuma za kudaiwa kukutwa na mtihani wa wa kidato cha nne.

Akizungumza  jana kuhusiana na tuhuma hizo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga Justus Kamugisha, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa suala hilo bado linaendelea na uchunguzi. 
 
Alisema kuwa uchunguzi wa tukio hilo utakapomalizika watatoa taarifa wa nini kimebainika.

Naye, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Mitihani Tanzania (Necta), Dk Charles Msonde alisema anachojua ni kwamba kuna walimu wawili wanaendelea kuchunguzwa dhidi ya tuhuma hizo, hivyo alishindwa kulizungumzia kwa undani hadi hapo watakapopatiwa taarifa na polisi.

Dk. Msonde alisema walipatiwa taarifa kutoka kwa wasamaria wema kuwa shule hiyo inadaiwa kuwa na mitihani.
 
Alisema walizifanyia kazi taarifa hizo na kuviarifu vyombo vya dola ambapo hatua zilichukuliwa dhidi ya washukiwa hao ili kubaini kama linaukweli au la.

“Baraza tunashindwa kuthibitisha tuhuma hizo kwa kuwa bado zinachunguzwa ila wadau wetu walitupatia taarifa na tunazifanyia kazi zitakapokamilika tutawajulisha,” alisema

Awali, chanzo chetu cha kuamini kutoka kituoni hapo kililiambia gazeti la Nipashe kuwa polisi walikwenda kufanya ukaguzi wao katika shule hiyo ambapo waliwashikilia walimu 12.

Baada ya uchunguzi wao walibainika walimu watatu kuwa na maswali kupitia simu zao za mkononi pamoja na majibu.

Mitihani huo ambao umemalizika hivi karibuni ulihusisha jumla ya watahiniwa 448,358 wa shule na wa kujitegemea uliofanywa nchi nzima ikiwa ni ongezeko la watahiniwa 150,870 kuilinganisha na watahiniwa 297,488 waliosajiliwa mwaka 2014.

Na Beatrice Shayo-Nipashe

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com