WANAFUNZI 8875 WAMECHAGULIWA KUJIUNGA KIDATO CHA KWANZA MKOANI RUKWA



 
WANAFUNZI wapatao 8,875 sawa na asilimia 55, ambao wamefaulu mtihani wa kumaliza elimu ya msingi, wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza katika shule za sekondari mbalimbali mkoani Rukwa.

Ofisa elimu mkoa wa Rukwa, Steven Mgina alisema hayo jana wakati wa kikoa cha kutangaza matokeo ya mtihani wa kumaliza elimu na uchaguzi wa wanafunzi wa kidato cha kwanza, kilichofanyika kwenye shule ya sekondari ya Kantalamba mjini hapa.

Mgina alisema kuwa kati ya wanafunzi hao 8,875 wavulana ni 4,939 na wasichana ni 3,936 kati ya watahiniwa 16,586 waliosajiliwa kufanya mtihani huo sawa na asilimia 60.15 ya walioandikishwa.

Alisema watahiniwa 516 sawa na asilimia 3 hawakuweza kufanya mtihani kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za utoro na mimba kwa wanafunzi wa kike.

Alisema kwamba kutokana na ufaulu huo mkoa umepanda kwa asilimia 8 ambao ni 55.25 ukilinganisha na ufaulu wa mwaka 2014 ambao ulikuwa asilimia 46.96 huku Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga ikiongoza kwa wastani wa asilimia 73.56 ikifuatiwa Nkasi, Sumbawanga vijijini na Kalambo ikiburuza mkia.

Mgina aliongeza kwamba kutokana na wanafunzi wote waliofaulu na kuchaguliwa kujiunga na elimu ya sekondari hivyo hakutakuwa na chaguo la pili (Second Selection) kama ilivyozoeleka.

Alisema hakuna sababu ya kufanya hivyo kwani wanafunzi wote waliofaulu wamepata nafasi ya kujiunga na kidato cha kwanza mapema mwakani.


Naye, Katibu tawala wa mkoa huo, SymthiesPangisa alisema licha ya ufaulu kuonyesha umepanda kwa asilimia nane, bado wadau wa elimu hawapaswi kujivunia kwa kuwa mkoa huo umeporomoka kutoka nafasi ya 19 mwaka 2014 hadi 23.


Alisema wataalamu wa sekta ya elimu ngazi ya mkoa, wanapaswa kutekeleza mara moja agizo la mkuu wa mkoa huo, Said Magalula la kwenda kujifunza katika mkoa jirani wa katavi ambao umefanya vizuri kiasi cha kushika namba moja kati ya mikoa 25 ya Tanzania bara.


Ikumbukwe kwamba Katavi ni mkoa uliozaliwa na Rukwa takribani miaka miwili iliyopita lakini kutokana na kuwa mikakati madhubuti katika sekta ya elimu imeweza kufaulisha wanafunzi wengi kiasi cha kushika nafasi hiyo.

Na Walter Mguluchuma-Malunde1 blog Sumbawanga.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post