JESHI la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limesema limeanza kuchukua hatua kali kwa watu waliohusika na upigaji wa picha wa vifaa vya kijeshi na kusambaza kwenye mitandao ya kijamii, ambapo hadi sasa tayari watu wanne wapo chini ya ulinzi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Habari na Mahusiano wa JWTZ, Kanali Ngemela Lubinga alisema kumekuwa na tabia ya kusambaa kwa taarifa, zisizotakiwa kusambazwa na kusababisha usumbufu kwa taasisi za Serikali na hasa Jeshi.
“Desemba 3, mwaka huu saa 1:15 jioni katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, lilitokea tukio lisilo la kawaida lililotendwa na wafanyakazi wa shirika la kupokea mizigo la Swiss Port wakishirikiana na wenzao wa Shirika la Ndege la KLM kwa kupiga picha vifaa vya kijeshi na kusambaza katika mitandao ya kijamii,” alisema Kanali Lubinga.
Alisema mizigo hiyo ni mali ya JWTZ na kuagizwa kwake, hakujaanza hivi karibuni kama baadhi ya watu katika mitandao ya kijamii wanavyoeleza, bali ni matokeo ya hatua zilizochukiliwa na JWTZ kupitia Wizara ya Ulinzi miaka sita iliyopita katika mpango wake wa kujenga uwezo wa JWTZ.
“Tunasikitika kwa tukio hili la watu kujichukulia maamuzi ya kupiga picha kitu ambacho hakikuwahusu na pia kusambaza picha hizo kwenye mitandao ya kijamii na kupelekea kujitokeza kwa maoni ya kupotosha jamii,” aliongeza Mkurugenzi huyo katika JWTZ.
Alisema tabia za kupotosha jamii, zimetokea mara kwa mara na hivyo kuvunja mshikamano uliopo kati ya Serikali na wananchi wake, jambo ambalo jeshi hilo halitalifumbia macho.
Alisema ni kwa msingi huo, wameanza kuwasaka wahusika wote, ambapo tayari watu wanne wapo chini ya ulinzi na watachukuliwa hatua kali ili iwe fundisho kwa wengine, kutokana na upigaji wa picha hizo na usambazaji wake.
Social Plugin