Mahakama ya Wilaya ya Mpanda imewahukumu watu wawili kifungo cha miaka 42 jela baada ya kupatikana na hatia ya kukamatwa na meno ya Tembo manne yenye thamani ya shilingi milioni 60.
Hukumu hiyo ilitolewa wiki iliyopita na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Mpanda Odira Amwol baada ya mahakama kuridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani na upande wa mashitaka.
Watuhumiwa hao waliohukumiwa kifungo hicho cha kwenda jela ni Justine Bruno(50) Mkazi wa Kijiji cha Usevya na Filiberti Leo(35) Mkazi wa Kijiji cha Ikuba wote wawili wakazi wa Wilaya ya Mlele Mkoa wa Katavi.
Awali katika kesi hiyo mwendesha mashitaka mwanasheria wa Serikali Jamila Mziray aliiambia Mahakama kuwa watuhumiwa hao wote wawili walikamatwa na meno ya tembo Novemba 17 mwaka huu majira ya usiku katika kijiji cha Ikuba Wilayani Mlele.
Siku hiyo ya tukio watuhumiwa hao walikamatwa na Askari wa jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi kwa kushirikiana na Askari wa TANAPA wa Mbuga ya Katavi huku wakiwa wamepakia kwenye pikipiki meno ya Tembo manne yenye uzito wa kilogramu 47.6 yenye thamani ya shilingi milioni sitini.
Upande wa mashitaka katika kesi hiyo ulikuwa na mashahidi watano na washitakiwa walikuwa hawana shahidi yoyote hivyo walijitetea wenyewe .
Hakimu Amwol kabla ya kusoma hukumu hiyo aliiambia Mahakama kuwa kutokana na mwenendo mzima wa kesi hiyo mahakama pasipo shaka yoyote imewatia washitakiwa hatiani hivyo kabla ya kutolewa kwa hukumu anawapa nafasi washitakiwa kama wanasababu yoyote ya msingi ya kuishawishi mahakama iwapunguzie adhabu anatowa nafasi kwa washitakiwa kujitetea.
Washitakiwa katika utetezi wao waliiomba Mahakama iwapunguzie adhabu kwa kuwa wanawazazi na watoto ambao wanaowategemea .
Mwanasheria wa Serikali alipinga vikali maombi hayo na kuiomba mahakama itowe adhabu kali kwa washitakiwa kwani tatizo la ujangili katika Mkoa wa Katavi limekuwa likiongezeka siku hadi siku hivyo wapewe adhabu ambayo itakuwafundisho na kwa watu wengine wenye tabia kama hizo.
Akisomo hukumu hiyo Hakimu Amwol aliiambia Mahakama kuwa washitakiwa wamepatikana na kosa la kuvunja sheria ya uwifadhi wa wanyama kifungu 86(1) 2b na c na kifungu cha sheria cha makosa ya kupanga na kuhujumu uchumi No 57 (1)(60) sura ya 200 marejeo ya 2002.
Hivyo kutokana na kupatikana na kosa hilo Mahakama imewahukumu Justine Bruno na Filiberti Leo kutumikia kifungo cha miaka 21 jela kwa kila mmoja .
Na Walter Mguluchuma-Malunde1 blog Katavi
Social Plugin