AFISA WA TAKUKURU AUAWA KWA KUPIGWA NA KUKATWA MAPANGA




OFISA wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCB) mkoani Dodoma, Emmanuel Meta (37) ameuawa kufuatia kupigwa na kukatwa mapanga na watu ambao mpaka sasa hawajafahamika.


Hata hivyo Jeshi la Polisi linamshikilia mtu mmoja kwa mahojiano zaidi kuhusiana na tukio hilo.


Tukio hilo lilitokea Januari 20, mwaka huu majira ya saa 6:15 usiku katika eneo la Area C manispaa ya Dodoma.


Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), David Mnyambuga, Ofisa huyo wa PCCB alifariki dunia wakati anapatiwa matibabu baada ya kupigwa na watu ambao hakuwafahamu.


Alisema mtoa taarifa wa awali wa tukio hilo, Athuman Mtengwa ambaye pia ni mfanyakazi PCCB, mkazi wa Area “D” alieleza kuwa, Januari 20, saa 6:15 usiku akiwa nyumbani kwake alipigiwa simu na Emmanuel (marehemu) ambaye ni mfanyakazi mwenzake pia ni rafiki yake wa karibu.


Alisema Meta alimweleza kuwa anaomba msaada wa kupelekwa hospitali kutibiwa kwa kuwa amepigwa na watu wasiofahamika wakati akirudi nyumbani kwake akitokea baa ya Rose Garden iliyopo Area “C” jirani na nyumbani kwake kwa matembezi.


Baada ya Mtengwa kufika alipiga honi ndipo Meta alitoka nje na kufunga mlango na geti kwa kufuli na kuingia katika gari kuelekea Hospitali ya Mkoa wa Dodoma na wakiwa njiani hali yake ilibadilika na kukosa nguvu na kushindwa kujimudu kwa lolote.


Alisema wakati akiendelea kupatiwa matibabu Hospitali ya Mkoa wa Dodoma alifariki dunia.


Kaimu Kamanda alisema uchunguzi wa mwili wa marehemu umefanyika ambapo amekutwa na jeraha kichwani linalovuja damu, alitokwa na damu puani na masikioni, uvimbe katika jicho la kulia na michubuko midogo mikononi.


“Mtu mmoja anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano zaidi na uchunguzi kuhusiana na tukio hilo unaendelea,” alisema Kaimu Kamanda.


Alitoa wito kwa mtu au watu wenye taarifa kuhusiana na tukio hili washirikiane na Jeshi la Polisi kuwafichua watu waliofanya uhalifu huo ili sheria ichukue mkondo wake.
Via>>Mpekuzi blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post