Zaidi ya wachungaji hamsini wa kanisa la Anglikana Tanzania dayosisi ya Victoria Nyanza (DVN) wametangaza kumfukuza kazi ya uaskofu, askofu Boniface Kwangu wa dayosisi hiyo kwa tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka na ubadhirifu wa fedha pamoja na mali za kanisa hilo.
Tamko hilo la wachungaji 53 wa dayosisi hiyo limesomwa mbele ya waumini wa kanisa kuu la mtakatifu Nicholas wakati wa ibada ya Jumapili na mchungaji Andrew Kashilimu, ambaye pia ni mwenyekiti wa nyumba ya wahudumu.
Kufukuzwa kazi ya uaskofu kwa askofu Boniface Kwangu aliyehudumu katika dayosisi hiyo ya Victoria Nyanza (DVN) kwa miaka minane, kuanzia mwaka 2008 hadi kufikia leo, kunafanya jumla ya maaskofu waliowahi kufukuzwa na kanisa hilo kufikia wawili, akiwemo mtangulizi wake marehemu John Changaye ambaye alifukuzwa uaskofu mwaka 2007 kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha na mali za kanisa hilo.
Askofu Bonifasi Kwangu amevuliwa wadhifa huo akiwa nchini Marekani ambako amekaa kwa zaidi ya mwezi mmoja.
Kanisa la Anglikana Tanzania dayosisi ya Victoria Nyanza (DVN) lina jumla ya wachungaji sitini na zaidi ya waumini laki sita katika makanisa yake.
Chanzo-ITV