CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimemtaka aliyekuwa mgombea urais wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, kutaja majina ya wafanyabishara aliodai wanaotozwa kodi kubwa na serikali kwa sababu walivisaidia vyama vya upinzani wakati wa kampeni.
Chama hicho kimesema endapo Lowassa asipofanya hivyo, lengo lake litakuwa ni kutaka kuigombanisha serikali iliyoko madarakani na wafanyabiashara wakubwa ambao ndiyo walipaji kodi wa nchi.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM (Taifa), Abdallah Bulembo, alisema endapo Lowassa asipowataja wafanyabishara hao atakuwa amesababisha wasiwasi mkubwa kwa wafanyabishara ambao waliwasaidia kipindi cha uchaguzi mkuu.
Aidha, Bulembo alisema madai hayo ya Lowassa yanaweza kusababisha wafanyabiasha hao ambao ndiyo wanaolipa kodi kuingiwa na wasiwasi wa kutozwa kodi kubwa na serikali.
Alisema masuala ya uchaguzi kwa sasa yameshamalizika hivyo Lowassa anapaswa kutaja majina ya wafanyabishara hao ambao anadai wanatozwa kodi kubwa kwa kukomolewa kwa sababu walivisaidia vyama vya upinzani.
“Maneno aliyayatoa Lowassa dhidi ya serikali yanaweza kudhoofisha kasi ya serikali ya Rais Dk. Magufuli ya kukusanya kodi. Kazi ya serikali ni kukusanya kodi, hivyo aiache ikusanye kodi kwa maendeleo ya taifa,” alisema na kuongeza:
“Lowassa ni mtu mkubwa sana hapa nchini, akisema neno linaweza kuleta madhara makubwa, hivyo anapaswa kutaja majina ya wafanyabishara hao kama wapo hata mia moja, ili watu wahoji kuwa awali walikuwa wanalipa kodi shilingi ngapi na hivi sasa wanatozwa shilingi ngapi.”
Bulembo aliongeza kuwa, kwa sasa serikali ya Rais Magufuli imeongeza makusanyo ya kodi kutoka Sh. bilioni 800 hadi kufikia Sh. trilioni 1.3, hivyo anapaswa kuungwa mkono badala ya kutoa kauli zinazoweza kumkwamisha.
SHULE ZA CCM
Aidha, Bulembo alisema shule 26 za Jumuiya ya Wazazi ya CCM, zilifanyiwa ukaguzi mwaka jana na kubainika 15 zina ubadhirifu wa fedha.
Alisema kutokana na hali hiyo, wahusika wote waliobainika katika kashfa hiyo watafikishwa katika vyombo vya sheria.
“Naomba wenyeviti wenzangu wa mikoa waache ukaguzi ufanyike, hatua zinazochukuliwa sasa ziendelee kuchukuliwa wala wasiogope na kutotoa ushirikiano ili wasije wakaingia katika migogoro,” alisema Bulembo.
Alisema hadi sasa kuna shule nne za jumuiya hiyo ambazo zimepelekwa mahakamani kutokana na ubadhirifu huo, hivyo viongozi walioko mikoani waone kinachotendeka kwa sasa ni halali na hakuna atakayeonewa.
Mwenyekiti huyo wa Jumuiya ya Wazazi CCM, Alisema miaka mitatu iliyopita wakati uongozi wake ukiingia madarakani, mapato kwa mwaka kutokana na miradi yake yote yalikuwa ni Sh. milioni 50, lakini kwa mwaka huu yameongeza na kuwa Sh. bilioni 1.6 kwa mwaka.
ADA ELEKEZI
Kuhusu ada elekezi, Bulembo alisema Jumuiya ya Wazazi ya CCM itaendelea kutoza ada kwa shule zake kwa kiwango cha zamani bila ya kufuata bei elekezi iliyotolewa na serikali.
Alisema CCM itakutana na serikali kuzungumzia suala hilo la ada elekezi kwa kuwa utekelezaji wake ni mgumu.
AMJIBU MAKONGORO MAKATIBU WAKUU
Bulembo alisema Rais Magufuli ameunda baraza la mawaziri lenye wizara 19 ikiwa ni idadi ndogo kuliko serikali iliyopita iliyokuwa na baraza la mawaziri 31.
Alisema kauli iliyotolewa na aliyekuwa Naibu wa Wizara ya Kazi na Ajira ambaye kwa sasa amehamia Chadema, Makongoro Mahanga, kuwa serikali hiyo ni kubwa kuliko iliyopita haina mashiko , kwani Rais Magufuli ameteua baraza la Mawaziri kwa kuzingatia ufanisi na utendaji makini.
Alisema Rais Magufuli ametimiza siku 60 tangu aapishwe kuwa Rais wa tano wa Tanzania, hivyo anapaswa kupewa muda wa kiutendaji zaidi.
Alisema kauli za vyama vya upinzani kudai kuwa Rais Magufuli anatekeleza ilani ya upinzani haina ukweli wowote, kwani mengi yamo ndani ya Ilani ya CCM likiwamo la kupambana na mafisadi na hata wakati wa kampeni zake alikuwa akieleza wazi.
Hivi karibuni vyombo vya habari vilimkariri Lowassa zungumza akiwa mkoani Tanga akidai serikali kuwatoza kodi kubwa wafanyabiashara waliokisaidia Chadema wakati wa kampeni na kuitaka CCM kuacha vitendo hivyo.
Lowassa alikaririwa akidai kuwa, imezuka tabia ya kuwanyanyasa wafanyabiashara waliounga mkono Chadema na kuitaka serikali ya Rais Dk. Magufuli iache mara moja.
CHADEMA WAZUNGUMZA
Msemaji wa Chadema, Tumaini Makene, alipotafutwa kulizungumzia suala hilo, alisema suala la kutaja majina siyo kazi yao.
Alisema Lowassa alichokieleza ni kuwa kuna mkakati wa serikali kushughulikia wafanyabiashara waliokuwa wanamuunga mkono wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana.
Alisema Chadema siyo kazi yake kutaja majina ya watu, bali inahitaji kuona Watanzania wote wanatendewa sawa bila ya ubaguzi wowote.
CHANZO: NIPASHE