MTU mmoja aliyejulikana kwa jina la David Igwesa, anayedaiwa ni daktari feki amekatamatwa katika Hospitali ya Mkoa wa Mwanza, Sekou Toure huku akiwa amemtapeli mgonjwa Sh. 170,000 kwa ajili ya kumfanyia upasuaji.
Daktari huyo feki amekamatwa leo saa 4 asubuhi katika hospitali hiyo, baada ya mgonjwa aliyetapeliwa fedha hizo kuanza kudai risiti za fedha alizotoa kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji.
Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk. Bahati Msaki, amesema taarifa za kuwepo daktari huyo feki zilianza kutolewa na wagonjwa wa hospitali hiyo kabla ya mgonjwa aliyetapeliwa, Dotto Chibula kutoa taarifa kwa uongozi husika.
Amesema kuwa daktari huyo alitiwa mbaroni kufuatia taarifa za kuwepo kwa daktari huyo feki na kwamba baada ya kumhoji alidai alikwenda katika hospitali hiyo kwa ajili ya kujifunza mafunzo ya vitendo kitendo ambacho ni cha uongo kwani uongozi wa hospitali haumtambui.
“Yeye anadai alikuja hapa kwa ajili ya kujifunza, taarifa zake za kujifunza sisi kama uongozi tulikuwa hatuna, tunao vijana wengi ambao wametoka Bugando (Hospitali ya Rufaa ya Bugando) wanaojifunza sasa huyo ametokea Bungando ipi.
“Kama uongozi mara nyingi tumekuwa tukitoa matangazo na kuwaeleza wagonjwa wanapotoa fedha zao wanapaswa kupewa risiti lakini utakuta mgonjwa anatoa fedha risti hawatoa, tunaomba wateja wote wawe wanaomba risiti,” amesema Msaki.
Msaki amesema kuwa baada ya kumhoji `tapeli` huyo hakuwa na zaidi cha kuzungumza licha ya kudai alikwenda hospitalini hapo kwa lengo la kujifunza hivyo taarifa za kwamba ni daktari katika hospitali hiyo sio kweli.
Mgonjwa anena
Tungu Chibula ambaye ni mtoto wa mgonjwa, Dotto Chibula, amesema kuwa awali kabla ya kutoa fedha hizo kwa daktari huyo feki, alikuwa anakwenda anamkuta katika wodi namba saba akiwa na daktari wengine.
Amesema zaidi ya mara tatu tangu afike hospitalini hapo amekuwa akimkuta daktari huyo feki akiwa na madaktari wengine wa Sekou Toure wakiendelea na uotaji wa huduma kwa wagonjwa hivyo alimuamini kumpata fedha hizo.
Amedai kuwa siku ya kwanza daktari huyo alimueleza kwamba ugonjwa wa baba yake ni mkubwa sana, hivyo kiasi cha fedha lazima kitakuwa kikubwa ambako alimwambia anapaswa kutoa Sh. 500,000 ndipo afanyiwe upasuaji.
Hata hivyo amesema kuwa baada ya kutajiwa kiasi hicho cha fedha, ambacho walikuwa hawana uwezo nacho walimuomba awapunguzie kwani kiasi hicho ni kikubwa sana, ambako aliwaambia wakatafute fedha kwanza wakirudi wataongea.
“Siku ambayo tulirudi (jana) tulikutana nae huyo huyo akatuambia atatupunguzia atatufanyia Sh. 500,000, ambako tulisema tuna Sh. 170,000, ambako tulimpatia na kutuambia nakwenda kuwachukulia risiti,” amesema Chibula na kuongeza.
“Pia kabla ya kumpatia hizo hela alichukua namba yangu ya simu kwamba atanipigia na muda mfupi baadae akanipigia akaniambia tukutane kwenye mgahawa wa hospitali nilienda na nikamkuta tukaongea ndipo tulikubaliana.”
Daktari feki
Kwa upande wake, daktari huyo feki, David Igwesa, amesema yeye katika hospitali hiyo hakuwa muuguzi bali alikwenda kwa ajili ya kujifunza huku akidai ametokea katika chuo kikuu cha Dodoma, hata hivyo alipotakiwa kuonyesha kitambulisho cha chuo alidai kimepotea.
Igwesa amesema kuwa yeye tuhuma zinazoelekezwa kwake hausiki nazo na kwamba tangu zamani alikuwa na ndoto za kuja kuwa daktari kwani huguswa na matatizo ya watu hususani wagonjwa.
Pia amesema kuwa katika kipindi chake cha mwezi mmoja katika hospitali hiyo ameona mambo mengi ikiwemo fedha nyingi wagonjwa wanazotoa zikipita katika mifuko ya nyuma na kwamba fedha nyingi hazifiki katika mfuko wa Serikali kwa ajili ya kuchangia pato la Taifa.
“Tangu niingie katika hospitali hii sasa yapata mwezi mmoja sasa, nimegundua kuna matatizo mengi, wagonjwa wanalipa fedha za kupatiwa huduma lakini hazifiki mahala husika, hivyo suala hilo linapaswa kuchunguzwa,” amesema Igwesa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Justus Kamugisha, alipotafutwa kuzungumzia juu ya suala hilo lilipofikia, simu yake ya mkononi haikuwa hewani.