Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DAR SI SALAMA...NI ROHO MKONONI,UKIBEBA FEDHA NYINGI UMEUMIA, BENKI SASA NI HATARI



NI roho mkononi. Hivyo ndivyo unavyoweza kusema kwa sasa juu ya hali ya usalama ilivyo katika Jiji la Dar es Salaam na maeneo kadhaa nchini pindi mtu anapokuwa amebeba kiwango kikubwa cha fedha.

Matukio ya ujambazi kwa kutumia silaha katika jiji hilo yamekuwa sugu na kusababisha wananchi wanaopeleka au kutoa fedha benki kuvamiwa, kujeruhiwa au kuuawa mchana kweupe na majambazi wanaotumia pikipiki aina ya Boxer.

Hali hiyo inawafanya watumiaji wa huduma za benki zilizo ndani ya jengo la Mlimani City maisha yao kuwa hatarini, hasa wale wateja wanaotoa fedha nyingi kutokana na kukumbwa na matukio ya kuuawa na kuporwa fedha.

Jengo hilo lenye matawi ya benki sita, limekuwa likikumbwa na matukio ya mauaji kwa wateja wanaotoa fedha nyingi na majambazi.

Matukio mengi ambayo yamekuwa yakitokea kwa wateja hao, majambazi wamekuwa wakitumia pikipiki aina ya Boxer ambayo ina uwezo mkubwa wa kukimbia.

Miongoni mwa matukio ya kusikitisha yakihusisha moja ya benki zilizopo Mlimani City ni lile lililotokea juzi ambapo mtu mmoja aliuawa na taarifa zake kuzagaa kwenye mitandao ya jamii.

Inaelezwa kuwa mtu huyo aliuawa na majambazi wakati akitoka kwenye moja ya benki ndani ya jingo hilo kuchukua kiasi cha Sh milioni 10 na kuanza safari ya kuelekea eneo la Tegeta Salasala ambako alikuwa akifanya shughuli za ujenzi wa nyumba yake.

Taarifa iliyosambaa mitandaoni inasema kwamba tukio hilo lilitokea jirani na mtoa taarifa hiyo aliyeamua kuwatahadharisha wananchi wengine kutochukua fedha nyingi katika benki zilizo eneo hilo.

Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo alisema kwamba mtu huyo alipotoa fedha hizo, majambazi walianza kumfuata kwa nyuma, wakampita na kumzuia kwa mbele.

“Majambazi walipomzuia kwa mbele walimtaka atoe milioni 10 aliyochukua benki, baada ya kutoa hiyo fedha ndipo walimpiga risasi,” alisema mtoa taarifa huyo ambaye hakupenda jila lake kutajwa .



MATUKIO MENGINE MLIMANI CITY

Taarifa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zinaeleza kwamba katika matukio hayo yanayotokea mfululizo, hivi karibuni maeneo ya Bamaga jirani na Hongera Bar, mtu mmoja na mkewe walivamiwa na majambazi walipokuwa wanatoka kuchukua fedha kiasi cha Sh milioni 13 katika benki mojawapo iliyopo Mlimani City.

Baada ya watu hao kuchukua fedha, majambazi yaliwafuata kuanzia hapo Mlimani City hadi Bamaga na kuwataka wawape fedha.

Inaelezwa kwamba jambo lililosaidia, mtu huyo alikuwa amezitenganisha fedha hizo na kuwapa laki 5, lakini walipatwa na hasira na kumhoji kuhusu fedha nyingine alikokuwa amezipeleka hali iliyofanya wampige risasi begani.

Hali hiyo ilimfanya mke wake awaongeze laki moja, na wakafanikiwa kubaki na kiasi kingine cha fedha walizokuwa wamezificha kwenye mlango wa nyuma.

Taarifa nyingine inaelezea kwamba mama mmoja aliyejulikana kwa jina la Mama Joshua alivamiwa na majambazi baada ya kuchukua fedha kiasi cha milioni 4 kwenye benki mojawapo ya Mlimani City.

Inaelezwa kwamba baada ya mama huyo kufika eneo la Kwa Kakobe, majambazi walimpita na kumsimamisha baada ya kujifanya kuwa wanamjua na aliposimama walimlazimisha kutoa kiasi hicho cha fedha alichokitoa benki na akawapa kunusuru maisha yake.

Kwa sasa benki zilizopo Mlimani City zinaonekana kuwa eneo hatari la kutolea fedha nyingi kutokana na taarifa kwamba upo uwezekano wa kuwapo kwa wafanyakazi wa baadhi ya benki hizo kushirikiana na majambazi.

Tukio jingine lilitokea mwaka jana na kushuhudiwa na gazeti hili, ambapo mtu mmoja alipigwa risasi mbili majira ya saa 6 mchana na kuporwa fedha akiwa katika gari maeneo ya Sinza Kijiweni karibu na Baa ya Deluxe.

Dereva aliyekuwa akiendesha gari hilo lililoshambuliwa namba T 236 DDT aliyefahamika kwa jina moja la Abasi, alisema fedha ambazo majambazi hao walichukua zilitolewa benki moja ya eneo la Mlimani City.

“Baada ya kuingia na kuegesha gari hapa jirani na hopitali hii ya watoto, alikuja mtu mmoja aliyekuwa amevaa koti jeusi akiwa ameshuka kwenye pikipiki aina ya Boxer na alipofika alisogelea gari letu na kufunua koti lake alilokuwa amebeba bunduki ya SMG,” alisema.

Alisema mtu huyo alimwelekezea silaha mtu aliyekuwa nyuma ya gari na kumwamuru kutoa fedha, lakini akaambiwa hakukuwa na fedha ndani ya gari.

“Baada ya kuona anabisha alimpiga risasi ya kwanza, akageuza SMG kwangu nikakimbia, akafyatua lakini hakunipata ndipo nikasikia risasi nyingine ikipigwa.

“Baada ya muda kulikuwa kimya na niliporudi tena nikakuta majambazi wakiwa wameshaondoka na mkoba wa fedha ‘briefcase’ na kutokomea nao hali iliyofanya wananchi kusogea na kumsaaidia mzee ambaye alikuwa amejeruhiwa vibaya kwa risasi,” alisema Abasi.

MTANZANIA ilipomuuliza dereva huyo kiasi cha fedha kilichoibiwa alisema majambazi hao waliondoka na kiasi kidogo cha fedha na si zote Sh milioni 10.

Tukio jingine lililotokea mwaka jana lilihusisha majambazi kumpora mama mmoja kiasi cha shilingi milioni 10 na kutokomea kusikojulikana.

“Alipotoka benki, majambazi hayo yalimfuata na kuligonga gari lake na ndipo dada huyo aliposimama ili aangalie nani kagonga gari yake ambapo jambazi mmoja alishuka na kumpiga risasi ya kifuani na kutokomea na kiasi hicho cha pesa,” alisema shuhuda wa tukio hilo.

Tukio jingine lilitokea eneo hilo Agosti 22, mwaka juzi likimuhusu Edson Cheyo mmiliki wa Kampuni ya Sowers African iliyopo jirani na Mlimani City aliyeporwa Sh milioni 18.

Cheyo alipigwa risasi ya kifuani na begani na majambazi waliomvamia wakiwa wamepanda pikipiki na walichukua fedha zote na mwenyewe kufariki dunia akiwa anapelekwa hospitali ya Mwananyamala.

Tukio jingine la mauaji ni lile la Sista Brigita Mbanga, mkazi wa Makoka pamoja na dereva Mack Patrick ambao waliuawa eneo la Ubungo Kibangu wakati wakitoka kuchukua fedha Mlimani City.



MTANDAO BENKI, MAJAMBAZI

Wananchi wamekuwa wakihoji ni kwa jinsi gani majambazi hao hupata taarifa za mtu aliyekwenda benki ama kuweka au kuchukua fedha.

Hata hivyo, imekuwa ikidaiwa kuwa baadhi ya benki nchini zimekuwa zikidaiwa kuajiri baadhi ya wafanyakazi walio kwenye mtandao wa majambazi kutokana na wateja wengi kupigwa risasi na kufa wakitoka kuchukua pesa.

“Haiwezekani hata mtu anapovamiwa na majambazi kabla ya kuuawa au kujeruhiwa huambiwa tupe miliooni 10 ambazo ndiyo zilizochukuliwa benki. Je, jambazi amejuaje kama wewe una kiasi hicho cha fedha?” alisema mmoja wananchi anayefanya shughuli zake Mlimani City.

Mkazi wa Tabata Kimanga, Dar es Salaam, Salum Mashati, alisema: “Haiingii akilini, utasikia mtu kaporwa fedha akitoka benki. Eti majambazi wanasema kabisa toa hizo milioni 20, wanajuaje kuwa una kiwango hicho? Huenda watu wa benki wanashiriki uhalifu huu.”



KAULI YA BENKI
Hata hivyo, meneja wa tawi moja la benki lililopo Mlimani City, ambaye hakupenda jina lake litajwe, alikanusha madai hayo na kusema hawana ushirikiano na majambazi hao wanaofanya uhalifu katika maeneo hayo.

“Si kweli kwamba benki zinashirikiana na majambazi kufanya uhalifu huu. Kwanza wahudumu (bank tellers) hawaruhusiwi kuingia na simu wanapohudumia wateja.



JESHI LA POLISI

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillus Wambura, alipotakiwa kuelezea namna polisi ilivyojizatiti kudhibiti matukio hayo yanayotokea katika benki hizo, alisema hakuna tukio hata moja ambalo limewahi kutolewa taarifa polisi.

“Hivi kweli inawezekanaje tangu kumeanza kutolewa taarifa hizo hakuna taarifa iliyowahi kutolewa polisi na mengi ya matukio ambayo yemekuwa yakiripotiwa yakifanyiwa ufuatiliaji yanakutwa ni uzushi, kwani hakuna tukio linalotokea hapa Dar es Salaam na wahusika walimalize kwa kukaa kimya,” alisema Kamanda Wambura.

Uchunguzi zaidi unaonyesha kuwa endapo hali hiyo haitadhibitiwa haraka, huenda wananchi wakapatwa na hofu ya kuweka fedha zao benki kwa kuogopa kuporwa na kupigwa risasi wakienda kuzichukua.

Hivi karibuni Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, DCP Simon Sirro, alikiri kuwapo kwa baadhi ya wafanyakazi wa benki wenye mtandao na majambazi, huku akisema jeshi lake limeweka mikakati kuhakikisha mtandao huo unasambaratishwa mara moja.

“Ni kweli kwamba baadhi ya mabenki, si yote, yameajiri baadhi ya wafanyakazi, si wote wenye mtandao na majambazi. Kwahiyo hata wao ni majambazi tu.

“Sasa tumejipanga vizuri ikiwa ni pamoja na kukamata pikipiki zinazohusika katika uhalifu. Pia tumeamua kuweka makachero nje na ndani ya mabenki, wapo polisi wa miguu, pikipiki na magari. Nina uhakika tutawadhibiti,” alisema Kamanda Sirro.

NA SHABANI MATUTU-MTANZANIA DAR ES SALAAM

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com