NB-Picha siyo ya mganga wa majambazi |
JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linamshikilia mganga wa kienyeji, Simba Said (44) mkazi wa Vingunguti Koloni, Dar es Salaam kwa tuhuma za kuwafanyia dawa majambazi kabla ya kwenda kufanya matukio ya uhalifu.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi Simon Sirro, alisema taarifa za kuwapo kwa mganga huyo walizipata kutoka kwa raia mwema.
Alisema baada ya kumkamata na kumhoji, alikiri kuwafanyia dawa watu wanaodaiwa kuwa majambazi.
“Mganga huyo aliyekamatwa eneo la Buguruni, alikiri kuwafanyia dawa majambazi ili wasikamatwe. Anasema amewafanyia dawa wengine ambao walikuwa wamejipanga kwenda kufanya uhalifu eneo la Buguruni,” alisema.
Alisema baada ya kupata taarifa hizo, waliweka mtego, lakini walipotaka kuwakamata majambazi hao walishtuka.
Kamanda Sirro alisema polisi walilazimika kuwarushia risasi na kufanikiwa kumjeruhi jambazi mmoja ambaye alipelekwa Hospitali ya Amana kwa ajili ya matibabu, lakini alifariki dunia.
Alisema majambazi wengine walifanikiwa kukimbilia eneo la Tabata wakitumia pikipiki tatu.
Aliwataja watuhumiwa hao ni Ibrahimu Mussa (40) mkazi wa Mbagala, Mohamedi Shaibu (20) mkazi wa Magomeni, Khamisi Jafari (44) mkazi wa Makambako na Abdulaziz Kikwanda (44) ambaye ni mlinzi na mkazi wa Buguruni.
“Wengine ni Juma Bakari (40) mkazi wa Majohe, Fitina Ramadhani (43) mkazi wa Magomeni Kagera, Dunia Rashid (50) mkazi wa Magomeni na Khamis Omary (36) Buguruni,” alisema Kamanda Sirro.
Wakati huo huo, jeshi hilo linamshikilia jambazi sugu Mkama Maiga (32) mkazi wa Mbagala Majimatitu aliyekuwa akitafutwa kwa muda mrefu.
Kamanda Sirro alisema mtuhumiwa huyo alipopekuliwa katika nyumba yake, alikutwa na bunduki aina ya Chinese ikiwa imefutwa namba zake.
HERIETH FAUSTINE NA MARTHA LUKUMAY-MTANZANIA DAR ES SALAAM
Social Plugin