Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Lucas Mkondya.
Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Joseph Mahende, amemuua mkewe, Musi Kitaleti, kwa kumkata kwa panga kisha kujisalimisha katika kituo cha polisi cha Sitakishari, jijini Dar es Salaam.
Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Jumatatu, wiki hii, katika eneo la Kwa Mpenda, Kata ya Kivule, Chanika wilayani Ilala.
Shuhuda wa tukio hilo ambaye ni mpangaji wa nyumba ya mtuhumiwa, Hellena Musa, aliiambia Nipashe kuwa wanandia hao walianza kugombana saa 5:45 usiku.
Alisema Mahende alifunga mlango wa geti, walipokuwa wanagomabana chumbani, ambapo alikuwa akimpiga mkewe na kitu chenye ncha kali.
“Walikuwa wanagombana mara kwa mara. Baada ya kuona ugomvi huo umechukua muda mrefu, tulikwenda kuchungulia dirishani kwake ndipo tukamwona anachoma mwilini kwa kutumia kitu chenye ncha kali ambacho kipo kama chuma,” alisema.
Aliongezea kuwa: “Walikuwa wakitoka chumbani na kukimbilia sebuleni. Tulishindwa kumwokoa huyu mama kwa kuwa mlango ulifungwa na jambo lingine ni kwamba huyu baba ni mkali hivyo tukawa tunaogopa,” alisema.
Kwa mujibu wa shuhuda huyo, ugomvi huo ulidumu kwa zaidi ya saa mbili na baada ya muda, alifanikiwa kutoka nje ambapo aliweza kupiga hatua tano na kuanguka na ndipo mtuhumiwa huyo alipomfuata na kumpiga na kitu chenye ncha kali kwenye kisogo.
Baada ya kufanya hivyo, alisema mtuhumiwa alichukua panga na kuanza kumcharanga mkewe kisogoni na hatimaye kupoteza maisha majira ya saa nane usiku.
Alisema baada ya kufanya hivyo, mtuhumiwa alimfunika mkewe na kwenda kupiga deki chumbani kwake kuondoa damu zilizokuwa zimetapakaa.
Shuhuda huyo alisema mtuhumiwa alikwenda kujisalimisha kituo cha polisi cha Sitakishari na baada ya muda mfupi, alirudi nyumbani na kuondoka tena ilipofika saa 12 asubuhi.
Gazeti hili lilizungumza na ndugu wa karibu wa mtuhumiwa ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, ambaye alisema tukio hilo limewasikitisha kwa kuwa alivyopatiwa taarifa hawakuamini kilichomkuta ndugu yao.
Alisema alipatiwa taarifa saa nane usiku wa kuamkia Jumatatu ambapo ilimbidi afike eneo la tukio kujionea hali ilivyokuwa.
Ndugu huyo alisema alipofika eneo la tukio, alikutana na kaka wa mtuhumiwa na mtuhumiwa mwenyewe ambapo walimwuliza ni kitu gani kilichomkuta na kueleza kuwa tayari ameshammaliza bila kutaka kutoa maelezo ya kile kilichosababishia.
Alisema anachoelewa ni kwamba watu hao wawili walikuwa na ugomvi wa muda mrefu, baada ya mtuhumiwa kuoa mke wa pili.
Kwa mujibu wa ndugu huyo, marehemu enzi za uhai wake alikuwa akidai apatiwe nyumba hali na baada ya kuona hatimiziwi matakwa yake, aliamua kufungua kesi mahakamani.
Hata hivyo, alisema mtuhumiwa alishakubali kutoa nyumba na kwamba kesi hiyo ambayo ilikuwa itolewe hukumu Januari 27, mwaka huu, alikuwa akabidhiwe hati ya nyumba kama aliyodai.
Licha ya kwamba suala hilo liko mahakamani, mkewe alikuwa akijitapa mtaani kuwa atahakikisha anamkomesha mumewe na kwamba akishapatiwa nyumba hiyo ataiuza.
“Huyu mkewe alishaambiwa anapatiwa nyumba lakini kila kukicha ni visa anaanzisha. Mara aende kazini kwa mumewe kumsemea maneno ya uongo. Pia kila mwezi mumewe alikuwa anakatwa Sh. 200,000 na kodi ya nyumba alikuwa anapokea lakini mumewe alipokuwa anarudi kutoka kazini, alikuwa hakuti chakula.
Naye Mjumbe wa Shina Na. 17 la mtaa huo, Jackson Mathayo, alisema kuwa tukio hilo limewaumiza na kwamba tatizo lililojitokeza ni kukosa taarifa kwa wakati.
Alisema alifika eneo la tukio na kushuhudia mwili huo ukiwa na majeraha sehemu mbalimbali za mwili huku maeneo ya kichwani yakiwa yamepasuliwa kwa panga.
Mathayo alisema mtuhumiwa baada ya kufika kituo cha polisi alirudishwa na kutakiwa kupeleka barua ya mjumbe inayothibitisha kuwa kafanya tukio hilo.
“Nimesikia kuwa alisema nimeua. Wale askari hawakuamini kwa kile alichokizungumza maana alikuwa anazungumza kama ni jambo jepesi na hakuwa na hofu ndiyo maana akaambiwa apeleke barua ya mjumbe,” alisema.
Baada ya kuambiwa hivyo, alisema alikwenda kwa balozi na kumweleza kuwa: “Mimi nimeshaua. Alipoulizwa tatizo ni nini alisema tayari ameua,” alisisitiza.
Mathayo alisema balozi hakuamini ikabidi amjulishe na mjumbe mwingine kwa ajili ya kwenda eneo la tukio kushuhudia suala hilo.
Alisema baada ya kushuhudia tukio hilo alipatiwa barua na kuipeleka kituo cha polisi ambapo wamemshikilia hadi sasa.
Naye Amina Sulemain ambaye ni jirani wa mtuhumiwa, mtuhumiwa huwa ana hasira za haraka, hivyo huenda mkewe alimpa majibu mabaya hali iliyosababishia kutokea kwa mauaji.
Mwili wa marehemu uliagwa jana saa sita mchana kwa ajili ya mazishi ambayo yatafanyika mkoani Mara. Familia ya mtuhumiwa haikusafiri na mwili wa marehemu kwa kuhofia huenda watalipiziwa kisasi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Lucas Mkondya, alipoulizwa kuhusiana na tukio hilo alikiri kutokea bila kulitolea ufafanuzi.
CHANZO: NIPASHE