MFANYABIASHARA maarufu wa mabasi ya kwenda mikoani anadaiwa kumficha mwanamke ndani ya shimo kwa zaidi ya mwaka mmoja.
Tukio hilo liligundulika Mbezi Luis Dar es Salaam jana, ambako ilidaiwa kuwa mwanamke huyo alikuwa amefichwa ndani ya shimo linalokadiriwa kuwa na urefu wa futi 10.
Kwa majibu wa mshuhuda wa tukio hilo, mmoja wa wapita njia alisikia sauti ya mtu ikitoka katika shimo lililokuwa jirani na nyumba ya mmiliki huyo wa mabasi na kuwaita watu waweze kushuhudia.
“Hili tukio ni la aina yake… inaelekea huyo dada yumo ndani ya hili shimo kwa zaidi ya mwaka, tena alikuwa akila unga maana mwili wake umedhoofika sana,” alisema mmoja wa mashuhuda ambaye hakupenda jina lake litajwe gazetini.
Vilevile, picha ya video ya mwanamke huyo zilionekana katika mitandao ya jamii jana zikimuonyesha akiwa mtupu.
Video hiyo iliwaonyesha polisi wakimuhoji mwanamke huyo ambaye alikuwa ajibu maneno yasiyoeleweka mithili ya mgonjwa wa akili.
Picha hizo zilikuwa zikimuonyeha mwanamke huyo akiwa anacheka na kuficha sura yake ili asionekane kwa watu waliokuwa katika eneo hilo, huku akiwa anajilaza chini na kuinuka.
Askari hao kwa kushirikiana na wananchi waliweza kumtoa ndani ya shimo hilo na kumpakia ndani ya gari kabla ya kumpeleka katika Kituo cha Polisi Mbezi.
Mmoja wa maofisa wa polisi wa Kituo cha Mbezi, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.
“Tukio hilo ni la ukweli na hata picha zipo zimesambazwa katika mitandao ya jamii zikionyesha kilichotokea,” kilisema chanzo chetu cha habari.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Polisi wa Konondoni, Christopher Fuime alipotafutwa alikanusha kuwapo tukio hilo.
“Ndugu mwandishi sina taarifa ya mwanamke aliyekutwa uchi,” alisema Kamanda Fuime kabla hata ya kuulizwa swali lolote na mwandishi .
Mwandishi pia alimtafuta Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro, ambaye alisema kuwa ndiyo alikuwa analisikia suala hilo kupitia kwa mwandishi.
Hata hivyo alisema angewasiliana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni kujua ukweli wa tukio hilo.
“Kwa kweli mimi sina taarifa hiyo wala hizo picha sijaziona, taarifa hii ndiyo naisikia kwako. Ngoja nitoe maagizo kwa RPC wa Kinondoni afuatilie tukio hilo kuweza kupata uhakika wa jambo hilo,” alisema Kamanda Sirro.
Baada ya saa moja MTANZANIA ilimtafuta tena Kamanda Fuime kujua kama alikuwa amekwisha kuzipata taarifa taarifa za tukio hilo lakini alisimamia kauli yake ya awali kwamba halikuwapo tukio lolote la mwanamke kukutwa shimoni Mbezi Luis.
Via>>Mtanzania