MKAZI mmoja wa Kijiji cha Mwamandi Kata ya Mwanase,katika Halmashauri ya Msalala,Wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga Marashi Lutaja amefariki dunia kisha kuzikwa pamoja na mali zake zote alizokuwa akimiliki katika familia yake,kutokana na mazingira ya kifo chake kuhusishwa na imani za Kishirikina.
Tukio hilo limetokea juzi katika kijiji hicho baada ya mwanakijiji huyo Mahushi Lutaja kufariki na baadaye familia yake kupitisha maadhimio ya kumzika na mali zake zote yakiwemo makreti ya bia na soda aliyokuwa akiyatumia kwenye baa yake,kwa imani ya kwamba kifo chake kimetokana na kulogwa nao kuhofia kwamba wakibaki na mali zake,watakumbwa na mauti.
Kwa mujibu wa diwani wa Kata ya Mwanase Samson Masanja, Lutaja baada ya kifo chake alizikwa na baiskeli 1 vitanda 4 na magodoro yake pamoja na masanduku ya nguo zake zote na vitu vingine vidogovidogo alivyokuwa akitumia
Pia Masanja alisema, Lutaja pia alizikwa na makreti ya bia na soda ambayo kabla ya kifo chake alikuwa akiyatumia kwenye biashara yake ya kuuza vinywaji kwenye kijiji hicho cha Mwamandi ambapo tukio hilo limehusishwa na imani za kishirikina
Wakati akiugua ndugu zake waliamini kwamba ugonjwa huo uliopelekea kifo chake ulitokana na kurogwa hivyo familia yake iliingiwa na hofu hiyo hasa kutokana na kuwepo madai ya waganga wa jadi kuamini kwamba ndugu yao alirogwa
Habari zaidi zinadai katika eneo hilo jamii ya huko inaimani na waganga wa jadi hivyo hata kifo hicho kutokana na familia ya marehemu kuamini waganga hao iliogopa kurithi mali za marehemu ambapo baadhi ya wananchi wa eneo hilo walidai kwamba chanzo cha ndugu hao kuziogopa mali hizo ni ushirikina.
Hata hivyo ndugu wa marehemu ambaye hakutaka kutaja jina lake,alidai kwa upande wa pesa marehemu alikuwa amemaliza kwenye akaunti yake kutokana na kusumbuka kujitibu kwa tiba za kitaalamu na zile za asili.
Afisa Mtendaji wa kata hiyo Nicholaus Lusana alisema kuna madai kwamba marehemu alirogwa kutokana na mali zake kupatikana kwa wizi ama njia zisizo halali hivyo ndugu zake waliamini kuwa ndugu yao amefariki kwa kurogwa na wenye mali aliowaibia marehemu
Kufuatia hali hiyo Lusana alisema Ndugu hao waliamini dawa zilizotumika kumloga ndugu yao zitawakumba na wao ndio sababu ya kumzika na mali zake zote kwa imani hiyo ambayo hata hivyo amewaonya wananchi wa eneo hilo kuachana nazo
Pamoja na hayo Lusana alisema anakwenda kijijini kuzungumza na familia hiyo na baadaye atatoa taarifa zaidi dhidi ya tukio hilo la aina yake ambalo limewashangaza wananchi wa wilaya ya Kahama na Jimbo la Msalala.
ENDELEA KUSOMA HABARI HII HAPA
Social Plugin