Mkazi wa Kijiji Cha Igagala Wilaya ya Mpanda Juma Sadi(50) amejinyonga hadi kufa kwa kutumia kamba ya chandarua baada ya kudai dawa za kienyeji alizokuwa amekunywa za kumzuia asife na mapema zimeishiwa nguvu.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Igagala Athumani Juma alisema tukio hilo lilitokea hapo juzi majira ya saa tano na nusu jirani na nyumba aliyokuwa akiishi marehemu.
Alisema marehemu kabla ya tukio alimweleza shemeji aitwaye Tanu Kabwe kuwa siku hiyo ya juzi lazima afe kwa kuwa aliwahi kumeza dawa za kienyeji(Mpigi) vipande vitatu ambayo ilikuwa ikimkinga asife na mapema na alikuwa ameisha vitapika vipande viwili vya dawa hizo hapo awali na siku hiyo ya juzi alikuwa ametapika(mpigi) yake ya mwisho hivyo hakuwa tena na kinga yoyote.
Na alimtaka shemeji yake ambaye muda huo walikuwa naye kwenye klabu cha pombe za kienyeji waende nae hadi nyumbani kwake ili akamkabidhi familia yake kwani yeye ilikuwa lazima afe siku hiyo.
Mwenyekiti huyo wa kijiji alieleza shemeji yake alipuuzia maneno hayo hali ambayo ilimfanya marehemu aondoke kwenye eneo hilo lililokuwa likiuza pombe ya kienyeji na kuelekea nyumbani kwake ambapo alikuta mkewe na kumwambia amwandalie uji ili anywe kwani alikuwa akisikia njaa .
Wakati mkewe akiwa anaendelea kuandaa uji marehemu alimwaga mkewe kuwa anatoka nje kwenda kufungia mbuzi na alitoka huku akiwa ameshika kamba ya chandarua mkononi mwake.
Alisema marehemu hakurejea tena ndani hadi majirani walipomwona akiwa amejinyonga hadi kufa huku akiwa amejifunga kipande cha kamba ya chandarua akiwa juu ya mti wa mwembe uliokuwa jirani na nyumba yake.
Majirani wa eneo hilo baada ya hapo walitoa taarifa kwa uongozi wa Serikali ya Kijiji ambao nao walitoa taarifa kwa jeshi la polisi ambao walifika kwenye eneo hilo na kisha mwili wa marehemu ulifanyiwa uchunguzi wa Kidaktari na kukabidhiwa ndugu kwa mazishi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi Dhahiri Kidavashari amethibitisha kutokea kwa kifo cha mtu huyo na jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi zaidi.
Na Walter Mguluchuma-Malunde1 blog Katavi
Social Plugin