Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira katika manispaa ya Shinyanga SHUWASA Mhandisi Sylivester Mahole akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu Januari 04,2016 akitolea ufafanuzi suala la kupanda kwa gharama za maji katika manispaa ya Shinyanga
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira katika manispaa ya Shinyanga SHUWASA Mhandisi Sylivester Mahole akizungumza na waandishi wa habari leo ofisini kwake kujibu malalamiko ya wananchi kuhusu kupanda kwa bei ya maji kutoka shilingi 790 kwa uniti moja na kufikia shilingi 1,105 kwa uniti moja kwa watumiaji wa majumbani pekee.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira katika manispaa ya Shinyanga SHUWASA Mhandisi Sylivester Mahole akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari leo(hawako pichani)
Mkurugenzi Mtendaji wa SHUWASA mhandisi Sylivester Mahole akizungumza na waandishi wa habari katika Bwawa la Ning'wa hivi karibuni baada ya waandishi wa habari kutembelea chanzo hicho cha maji kwa ajili ya wakazi wa Manispaa ya Shinyanga
Sehemu ya kutibu maji yanayotoka katika bwawa la Ning'wa
*********
Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira katika manispaa ya Shinyanga SHUWASA imewafukuza kazi watumishi wake 12 kwa makosa mbalimbali ikiwemo rushwa,ukosefu wa nidhamu kazini na kutengeneza takwimu hasa wanapokwenda kusoma mita za wateja wa mamlaka hiyo.
Hayo yamesemwa leo na mkurugenzi wa SHUWASA Mhandisi Sylivester Mahole wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga.
Mahole alisema walikuwa wanapata malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu baadhi ya watumishi wa mamlaka hiyo hususani wale wanaosoma mita kukadiria uniti za maji walizotumia wateja wao na kusababisha kuwa na mtazamo hasi kwa mamlaka hiyo.
“Kuanzia Mwezi Julai hadi Desemba mwaka 2015 tumefukuza kazi watumishi 12 kutokana na sababu ya kupika takwimu(data),walikuwa wanakaa chini ya mti bila kufika kwa wateja na kutengeneza takwimu,lakini pia walikuwa wanaendekeza vitendo vya rushwa na dhambi zingine nyingi zilizowafanya wananchi wawe na mtazamo hasi kwa mamlaka hii”,alieleza Mahole.
Aliongeza kuwa baada ya kuwatimua kazi watumishi hao waliajiri watumishi wengine 22 mwezi Agosti mwaka 2015 ili kuhakikisha nidhamu kwa watumishi wa mamlaka hiyo inakuwepo.
Katika hatua nyingine Mahole alisema mamlaka hiyo imeongeza bei ya maji kwa wateja wake kutoka shilingi 790/= kwa uniti moja hadi shilingi 1105/= kwa uniti moja ili kusaidia mamlaka ijiendeshe,lakini pia kuongeza nafasi ya uwekezaji na kupanda kwa gharama za vifaa vya kutolea huduma ya maji ikiwemo dawa za kutibu maji.
Mhandisi Mahole alifafanua kuwa bei hiyo ya maji imekuja baada ya EWURA na SHUWASA kuwashirikisha wateja wao kwa kufanya mikutano tangu mwezi Mei mwaka 2015 lengo likiwa ni SHUWASA kuweza kuboresha mtandao wake wa maji na fedha hizo haziendi sehemu yoyote zaidi ya maboresho na ukarabati.
"Tuliomba kuongeza bei kwa uniti moja kuwa shilingi 1,474/=,tukafanya mkutano na wananchi na EWURA wakiwepo lakini EWURA ikaelekeza shilingi 1,105/=kwa uniti moja,hii bei siyo kubwa kulingana na hali halisi ya maisha ya sasa,tunaomba wananchi waelewe kuwa sisi tunafanya kazi kwa kuzingatia maoni ya wananchi wala siyo vinginevyo",alieleza Mhandisi Mahole.
Hata hivyo kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu watumishi wa SHUWASA kutozingatia maadili ya kazi yao kwani baadhi yao wanaendekeza vitendo vya rushwa hasa maji yanapokatwa,kusoma mita kwa kukadiria na ongezeko la bei ya maji bila kushirikishwa.
Mhandisi Mahole SHUWASA amekutana na waandishi wa habari mkoa wa Shinyana ikiwa ni siku chache tu baada ya madiwani wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika manispaa ya Shinyanga kutishia kufanya maandamano huku wananchi wakiwa wamebeba ndoo kichwani kupinga ongezeko hilo la bei ya maji.
Madiwani hao wa Chadema wakiongozwa na mwenyekiti wao Emmanuel Ntobi walikutana na waandishi wa habari kuhusu nia yao ya kufanya maandamano kupinga ongezeko la bei ya maji..SOMA HABARI KUHUSU TAMKO LAO HAPA
Na Kadama Malunde-Malunde1 blog Shinyanga
Na Kadama Malunde-Malunde1 blog Shinyanga
Social Plugin