Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

KUHUSU WATUMISHI 6 WA SERIKALI KUTIWA MBARONI HUKO KAHAMA



Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Mika Nyange


WATUMISHI sita wa Halmashauri ya Mji wa Kahama mkoa wa Shinyanga, wamekamatwa na Polisi.


Wafanyakazi hao ni miongoni mwa waliosimamishwa kazi hivi karibuni na wengine kuwekwa katika uangalizi maalumu kwa tuhuma za kula njama za kujipatia zaidi ya Sh milioni 800, zilitolewa na Mgodi wa dhahabu wa Buzwagi.


Fedha hizo zilitolewa na mgodi huo kwa lengo la kutekeleza miradi ya maendeleo ya wananchi wa halmashauri hiyo.


Waliokamatwa ni Katibu wa Bodi ya Zabuni, Joseph Maziku ambaye ni Ofisa Ugavi na Wajumbe, Kulwa Ntaudyimara (Ofisa Utumishi) na Annastazia Manumbu (Ofisa Elimu Sekondari).


Wengine ni Joachim Henjewele ambaye ni Mkuu wa Idara ya Ardhi, Elius Mollel, Ofisa Biashara na Gervas Lugodisha kutoka Ofisi ya Ugavi.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga Mika Nyange, alikiri kukamatwa kwa watumishi hao.


Alieleza kuwa leo atatoa ufafanuzi juu ya hatua iliyofikiwa kuhusu tuhuma za watumishi hao, baada ya kuwasiliana na Mkuu wa Polisi wa wilaya ya Kahama.


Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Anderson Msumba, alisema watumishi hao walikamatwa juzi na Polisi baada ya kampuni moja, kati ya kampuni nyingi zilizohusika katika fedha hizo, kujitokeza katika ofisi za halmashauri kudai malipo, wakati nyaraka zake zinapishana na za kampuni iliyopewa kazi na Bodi ya Zabuni.


Nyaraka za Halmashauri zinaonesha kuwa Bodi ya Zabuni iliipa kazi Kampuni ya Noble Cliff Construction na kuonesha malipo yatafanyika kupitia akaunti ya benki ya NMB, huku madai ya kampuni hiyo yalionesha kulipwa fedha kupitia Benki ya Afrika (BOA).


Baada ya kuwepo mabishano ya kutofautiana kwa mikataba, Msumba alidai alimtuma Mweka Hazina wake kwenda kukagua akaunti hizo na kukuta ile ya BOA, ambayo kampuni hiyo ilidai ilipwe, ilishafungwa siku nyingi na ya NMB ambayo ilipitishwa na Bodi ya Zabuni, ilikuwa ikimilikiwa na mtu binafsi.


Msumba alidai hali hiyo ilionesha kulikuwa na kasoro katika mchakato wa utoaji wa zabuni. Wajumbe wote wa Bodi ya Zabuni ya Halmashauri ya Mji wa Kahama, wamekamatwa kutokana na sakata hilo na hadi jana walikuwa mahabusu katika Kituo Kikuu cha Polisi cha wilaya.


Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Vita Kawawa alitoa tuhuma kuhusu fedha hizo za Buzwagi katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo hivi karibuni.

Baada ya hapo, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Abel Shija, aliwasimamisha kazi watumishi watano kwa tuhuma hizo za kutumia vibaya fedha za Mgodi wa Buzwagi. Aliagiza waliohamishwa na wanatuhumiwa, warejeshwe kujibu tuhuma zao.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com