Miili ya marehemu Marco Martine(29) kushoto na Paskaline Nikomedi(26) baada ya kupigwa na shoti ya umeme katika nyumba ya mzee Zabron Mazoya ambayo haina huduma ya umeme katika mtaa wa Bondeni kata ya Masekelo maarufu kwa jina la Upongoji mjini Shinyanga-Picha zote na Kadama Malunde-Malunde1 blog
Mwenyekiti wa mtaa wa Bondeni kata ya Masekelo Mohammed Hizza Saguti akielezea jinsi tukio lilivyotokea
Mwenyekiti wa mtaa wa Bondeni kata ya Masekelo Mohammed Hizza Saguti akionesha sehemu ambayo ulikuwa umefungwa waya kwa ajili ya kuanikia nguo,ambao unadaiwa kusababisha vifo vya watu wawili
Kushioto ni Diwani wa kata ya Masekelo Samwel Sambayi akizungumzia tukio hilo ambapo amewataka wananchi kusubiri uchunguzi ufanyike ili kubaini chanzo cha vifo hivyo badala ya kukimbilia kuamini kuwa ni imani za kishirikina.
Wananchi wakiwa eneo la tukio
Kushoto ni bwana Paul Maduhu jirani aliyekuwa wa pili kufika eneo la tukioa, aliyenusurika kifo katika tukio hilo akionesha mahali palipotokea tukio hilo na kueleza kuwa baada ya kufika katika nyumba hiyo alikuta watu hao wameanguka chini huku waya uliokuwa unatumiwa kuanikia nguo ukitoa cheche za moto huku miili ya marehemu ikitoa moshi.
Mwenyekiti wa mtaa wa Bondeni kata ya Masekelo Mohammed Hizza Saguti akionesha waya wa Cable(TV) ambao unadhaniwa kuwa huenda ndiyo umesababisha shoti hiyo,uliopita nyuma ya nyumba ya mzee Zabron Mazoya kuelekea nyumba ya jirani
Mwenyekiti wa mtaa wa Bondeni kata ya Masekelo Mohammed Hizza Saguti akionesha nyaya za cable ambazo huenda ndiyo sababu ya shoti ya umeme
Nyuma ya nyumba ya mzee Zabron Mazoya,kushoto ni nyumba ya jirani yake,ambayo ina umeme,ambapo baadhi ya wakazi wa eneo hilo wamesema huenda kuna watu walikuwa wanatumia umeme kwa njia ya wizi
Nyumba za mzee Zabron Mazoya,juu ni nyaya za cable ya Tv zinadaiwa kuwa huenda ni chanzo cha shoti hiyo
Waya wa Cable ya TV ukiwa juu ya nyaya za umeme wa TANESCO ambazo zinadaiwa kuwa chanzo cha shoti ya umeme katika nyumba ya mzee Zabron Mazoya
Wananchi wakionesha waya mwingine wa kuanikia nguo katika nyumba hiyo
Mzee Zabron Mazoya mgonjwa wa mguu wa kushoto ,mmiliki wa nyumba akionesha taa/tochi anayotumia wakati wa usiku kwani nyumba zake zote hazina huduma ya umeme.
Nyumba ya kubwa ya mzee Zabron Mazoya,nyuma yake ni nyumba zake zingine ambapo alikuwa na mpangaji mmoja pekee Paskaline aliyefariki kwa kile alichodai katika mazingira ya kutatanisha
Kulia ni Mzee Zabron Mazoya akielezea juu ya tukio hilo
********
Kumetokea tukio la aina yake leo saa moja asubuhi mjini Shinyanga,ambapo kwatu wawili wamefariki dunia katika mazingira ya kutatanisha kwa kile kinachotajwa kuwa ni shoti ya umeme kwenye nyumba isiyokuwa ya umeme mali ya mzee Zabron Mazoya iliyopo mtaa wa Bondeni kata ya Masekelo maarufu Upongoji katika manispaa ya Shinyanga.
Malunde1 blog imefika eneo la tukio kwani huwa hatupitwi na matukio,ambapo wananchi wa eneo hilo wameonesha kushangazwa na tukio hilo kwani waya uliosababisha vifo hivyo ulikuwa unatumika kuanikia nguo pekee na nyumba hiyo haina huduma ya umeme,huku wengine wakidai huenda shoti imesababishwa na nyaya/Cable kwa ajili ya runinga zilizopita juu ya nyumba hiyo kuelekea nyumba ya jirani.
Waliofariki dunia ni Paskaline Nikomedi(26) aliyekuwa anafua nguo na kuanika nguo kwenye waya na Marco Martine(29) aliyefika eneo la tukio kumsaidia jirani
Mmiliki wa nyumba hiyo mzee Zabron Mazoya ambaye ni mgonjwa wa mguu kwa muda mrefu,ameiambia Malunde1 blog kuwa alisikia kelele za mpangaji wake Paskaline Nikomedi (26)akiomba msaada na majirani walipofika walikumkuta mpangaji huyo ameanguka chini na katika kutoa msaada jirani aliyejulikana kwa jina la Marco Martin(29) alipogusa tu mwili wa binti huyo naye alianguka kisha mwili wake kuanza kutoa moshi wakapoteza maisha papo hapo.
Mazoya amesema tukio hilo siyo la kawaida kwani nyumba yake haina umeme,na kushangaa kuona shoti ya umeme inatokea nyumbani kwake hivyo huo ni uchawi na ushirikina tu na kuongeza kuwa waya uliosababisha vifo wamekuwa wakiutumia kwa muda mrefu na hata jana jioni waliutumia kuanikia nguo.
“Zimamoto wamefika hapa,wafanyakazi wa Shirika la Umeme nchini TANESCO nao wamefika,lakini wameshindwa kuelewa chanzo cha tukio hili,wamesema watarudi tena kwa vile katika eneo hili wamekata umeme”,amesema mwenyekiti wa mtaa wa Bondeni Mohammed Saguti.
Diwani wa kata ya Masekelo Samwel Sambayi amewataka wananchi kusubiri uchunguzi ufanyike ili kubaini chanzo cha vifo hivyo badala ya kukimbilia kuamini kuwa ni imani za kishirikina
kwani huenda kuna watu wamejiunganishia umeme kinyemela au hizi nyaya za runinga zinazopita juu ya nyumba zilizogusa bati.
Meneja wa TANESCO mkoa wa Shinyanga Injinia Felix Olang amesema bado wanaendelea kufanya uchunguzi juu ya tukio hilo kwani linachanganya kutokana na nyumba hiyo kutokuwa na chanzo chochote cha umeme na kwamba wataalam wa umeme kutoka TANESCO wamefika kwenye nyumba hiyo na kubaini kuwa haina haya nyaya moja ya umeme.
Kamanda wa jeshi la zimamoto mkoa wa Shinyanga Elisa Mugisha amesema wamefika eneo la tukio kwa kushirikiana na TANESCO na bado wanaendelea kufanya uchunguzi ili kubaini chanzo cha tukio hilo kwani nyumba hiyo haina huduma ya umeme huenda kuna watu walijiunganishia umeme.
Hata hivyo baadhi ya wakazi wa eneo hilo wamesema tukio hilo ni la kishirikina kwani eneo hilo la mtaa wa Bondeni maarufu Upongoji linasifika kwa vitendo vya kishirikina hivyo hawashangai sana kuona shoti ya umeme inatokea mahali pasipo na umeme,na kuziomba mamlaka zinazohusika kufanya uchunguzi ili kubaini chanzo cha uhakika cha vifo hivyo.
Mwandishi mkuu wa Mtandao huu ,Kadama Malunde,bado anafuatilia undani wa tukio hili,tutakuletea taarifa zaidi hapa hapa,endelelea kutembelea Malunde1 blog,Fahari ya Shinyanga
Social Plugin