Johari akiugulia maumivu makali kutokana na jeraha alilolipata-Picha zote na Victor Bariety-Malunde1 blog Geita
Johari akiwa haamini kilichotokea muda mfupi baada ya kupatiwa huduma ya kwaanza hospitali ya mkoa wa Geita
Wananchi wakiangalia majeraha aliyopata johari muda mfupi baada ya ajali hiyo mjini Geita
Askari polisi kikosi cha usalama barabarani wilayani Geita aliyefahamika kwa jina la Charles mwenye cheo cha meja,juzi alinusurika kipigo kutoka kwa wananchi wenye hasira kali baada ya kumpiga na fimbo mgongoni mwendesha pikipiki aliyekuwa mwendo kasi na kutaka kusababisha kifo cha mwanamke Johari Issa(27)aliyekuwa amebebwa kwenye pikipiki hiyo ambaye alidondoka na kujeruhika vibaya.
Tukio hilo limetokea Januari 5,2016 majira ya asubuhi katikati ya mji wa Geita kwenye barabara kuu ya rami itokayo chato kwenda jijini Mwanza wakati mwendesha pikipiki huyo ambaye hakuweza kufahamika jina lake mara moja akitokea maeneo ya ‘msalala road’ kwenda stand ya mabasi ya mkoani ambako alikuwa akimpeleka abiria wake huyo.
Mashuhuda wa tukio hilo waliieleza Malunde1 blog kuwa,Trafiki huyo huku akiwa na fimbo mkononi alitoka upande wa pili wa barabara alikokuwa amesimama kuzuia watu kukatiza barabara hiyo hadi hapo msafara wa makamu wa Rais Samia Suluhu aliyekuwa kwenye kikao ukumbi wa halmnashauri ya mji wa Geita utakapopita na kuanza kumpiga nayo mgongoni mwendesha pikipiki huyo bila kujali alikuwa kabeba abiria hali iliyopelekea mwanamke aliyekuwa amebebwa kudondoka na kuviringika kwenye rami zaidi ya mara mbili huku bodaboda naye akikimbia kuokoa maisha yake.
‘’Yule trafiki alikuwa anapanga watu wasikatize barabara hadi msafara wa makamu wa Rais utakapopita na ndiyo akatokea huyo bodaboda akiwa hana hili wala lile na abiria wake,na ndipo yule Trafiki akakurupuka kutoka upande aliokuwa na kumfuata yule bodaboda na kuanza kumchapa na fimbo mgongoni na kusababisha apoteze uelekeo hali iliyosababisha kumdondosha abiria wake huyo ambaye aliviringika kwenye rami na kuumia vibaya na kama kungekuwa na gari inakuja ingemgonga na kumuua maana alidondokea katikati ya rami’’alisema James Bugomola shuhuda wa tukio hilo.
Alisema baada ya tukio hilo wananchi walikwenda kumbeba na kumtoa barabarani mwanamke huyo kupisha msafara wa makamu wa Rais ambao kwa wakati huo ulikuwa unapita huku trafiki huyo akitokomea kusikojulikana baada ya wananchi kuanza kuvuka barabara kumfuata alikokuwa.
Kwa upande wake Johari Issa(27)akiongea na Malunde1 blog mbali na kusikitishwa na tukio hilo alidai kuwa, bodaboda huyo alikuwa akimtoa maeneo ya mtaa wa msalala road anakoishi kwenda stand ya mabasi ya mikoani ya mjini Geita ili akapande basi kuelekea jijini Mwanza,kabla ya ajali hiyo ambayo ilikatisha safari yake kwa ajili ya kushughulikia matibabu kutibu majeraha aliyoyapata.
‘’Nilikuwa natoka nyumbani kuelekea stand ili nikapande basi kwenda mwanza na nilipofika eneo nililosababishiwa ajali,Trafiki alimfuata bodaboda wangu na kuanza kumtandika bakora mgongoni na ndipo alipopoteza uelekeo na kunidondosha mimi hadi nikaumia kama unavyoona’’alisema Issa akiwa katika hospitali ya Mkoa wa Geita akisubili matibabu.
Hata hivyo alisema tayari ametoa taarifa kwa wakubwa wake wa kazi ikiwa ni pamoja na kumchukua maelezo,kumpatia fomu namba tatu kwa ajili ya matibabu na wameahidi kuyafanyia kazi malalamiko yake dhidi ya askari huyo.
Mtandao huu ulifika ofisi ya kamanda wa polisi mkoa wa Geita Latson Mponjoli lakini halikumkuta kutokana na ugeni wa makamu wa Rais,lakini mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai SP Kayumba alikiri kupokea malalamiko ya mwanamke huyo na kuahidi kuyafanyia kazi.
‘’Huyu mwanamke amefika hapa na nimemuona mwenyewe nikaagiza achukuliwe maelezo na apatiwe fomu namba tatu kwa ajili ya matibabu na ameshashughulikiwa na tutachukua hatua kwa askari huyo’’alisema RCO Kayumba.
Aidha baadhi ya wananchi mkoani Geita wamemtaka kamanda wa polisi mkoa wa Geita Latson Mponjoli kumwajibisha askari huyo mwenye cheo cha meja kwa kosa la kumsababishia ajali mwanamke huyo huyo ili liwe fundisho kwa wengine wenye tabia ya kukurupuka kama yeye ambapo mbali na kukatisha safari ya mwanamke huyo na kunusurika kufa amemsababishia maumivu na majeraha sehemu za mwili wake.
Na Victor Bariety-Malunde1 blog Geita