Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Helen Malembeka (40) Mkazi wa Kijiji cha Ikuba Tarafa ya Mpimbwe Wilaya ya Mlele Mkoani Katavi ameuawa kwa kukatwa katwa na mapanga kichwani na shingoni wakati akiwa anaendesha pikipiki.
Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Katavi Dhahiri Kidavashari alisema tukio hilo limetokea juzi katika Kitongoji cha Usumbura Kijiji cha Ikuba.
Alisema siku hiyo ya tukio marehemu alikuwa akiendsha pikipiki aina ya Toyo yenye rangi nyekundu isiyokuwa na namba za usajili .
Alikuwa akitokea Kijiji cha Usevya Tarafa ya Mpimbwe akiwa anaelekea nyumbani kwake katika Kitongoji cha Usumbura ndipo akiwa njiani alivamiwa na watu wasiojulikana na kufanyiwa mauaji hayo.
Kamanda Kidavashari alisema wauaji hao baada ya kufanya mauaji walitokomea kusikojulikana na kuiacha pikipiki hiyo ya marehemu Helen Malembeka bila kuichukua.
Alisema mpaka sasa chanzo cha mauaji hayo bado hakijafahamika na upelelezi wa tukio hilo unaendelea kwa polisi wakiwa wanashirikiana na wakazi wa eneo la Kijiji cha Ikuba ili kubaini sababu zilizosababisha mauaji hayo.
Kidavashari aliwaambia waandishi wa Habari kuwa mpaka sasa hakuna mtu wala watu walioshukiwa na kukamatwa kuhusiana na tukio hilo .
Hilo ni tukio la nne kwa kipindi cha siku nne kutokea kwa mauaji ya aina hii ya watu kuuawa katika Mkoa wa Katavi na watu wanaofanya vitendo hivyo kuuwa na kutochukua kitu chochote cha marehemu hao .
Na Walter Mguluchuma-Malunde1 blog Katavi
Social Plugin