Baada ya mapumziko ya siku moja kutokana na kukamilisha hatua ya Makundi ya michuano ya Kombe la Mapinduzi kwa mwaka 2016, January 10 michuano ya Kombe la Mapinduzi iliendelea katika hatua ya nusu fainali. January 10 saa 16:15 ulipigwa mchezo wa kwanza wa nusu fainali kati ya Simba dhidi ya Mtibwa Sugar, wakati nusu fainali ya pili ikipigwa saa 20:15 usiku.
Mchezo wa nusu fainali ya kwanza kati ya Mtibwa Sugar dhidi ya Simba ulikuwa ni mchezo wa kuvutia kwa kiasi kikubwa na ulianza kwa timu zote kucheza mpira wa taratibu na kuusoma mchezo, Mtibwa walipata goli la ushindi dakika ya 45 baada ya Chiza Kichuya kupiga shuti kali lililomfanya Peter Manyika kutema na Ibrahim Jeba kupachika goli la ushindi.
Hadi dakika 90 zinamalizika Simba hawakufanikiwa kusawazisha goli, na kufanya mchezo kumalizika kwa Mtibwa Sugar kutinga fainali kwa ushindi wa goli 1-0. Kwa matokeo hayo Mtibwa Sugar wametangulia fainali na sasa wanasubiri mshindi wa mchezo wa nusu fainali ya pili kati ya Yanga dhidi ya URA ya Uganda.
Social Plugin