POLISI ASHUSHIWA KIPIGO KISHA KUPORWA BUNDUKI NA WANANCHI MNADANI


NB-Picha haihusiani ha habari hapa chini



WANANCHI wa Wilaya ya Kiteto, mkoani Manyara, wamempiga askari polisi na kumpora bunduki aina ya SMG.

Tukio hilo lilitokea jana saa saba mchana katika mnada wa Dosidosi, wakati askari huyo alipokuwa akitaka kumwokoa mtuhumiwa mmoja aliyekuwa akishambuliwa na wananchi mnadani hapo.

Polisi aliyeporwa bunduki hiyo, ametajwa kwa jina la PC Ginue anayefanya kazi katika Kituo cha Polisi Kibaya (Kiteto).

Taarifa zilizopatikana kutoka kwa walioshuhudia tukio hilo, zinasema polisi huyo alimwokoa mtu huyo ambaye alikuwa akituhumiwa kuiba Sh 800,000.

Mmoja wa mashuhuda hao alisema mtuhumiwa huyo ambaye hakupatikana jina lake, alimpora fedha hizo mmoja wa wafanyabiashara wa ng’ombe na kukimbia nazo.

“Baada kupora fedha huyo mtu alikimbia nazo, lakini alikamatwa na kuanza kushambuliwa kwa silaha za jadi.

“Wakati mtuhumiwa huyo akishambuliwa na wananchi waliokuwa wamejaa hasira, askari polisi waliokuwa mnadani hapo kwa ajili ya kuimarisha ulinzi, walijitokeza na kutaka kumwokoa kwa kupiga risasi za moto hewani.

“Baada ya kupiga risasi hizo, walisogea eneo la tukio wakiwa na gari aina ya Noah na kumpakia mtuhumiwa kwenye gari haraka na kuondoka naye wakielekea Kibaya ambako ndiko yaliko makao makuu ya Wilaya ya Kiteto.

“Wakati askari hao wanaondoka na gari hilo, PC Ginue alichelewa kupanda gari hilo, kwa hiyo wananchi walimvamia na kuanza kumshambulia kwa fimbo la silaha za jadi.

“Walipofanikiwa kumzidi nguvu, walimpora bunduki aliyokuwa nayo na kutokomea nayo kusikojulikana,” alisema mtoa taarifa huyo.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Dosidosi, Juma Maganga, alithibitisha uwepo wa tukio hilo na kusema waliopora bunduki hiyo wanatafutwa.

Pia, alisema wakati polisi huyo alipokuwa akishambuliwa, watu watatu walijeruhiwa na kukimbizwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kiteto kwa matibabu zaidi.

Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Samuel Nzoka, pamoja na kuthibitisha uwepo wa tukio hilo, aliwataka wananchi kutoa ushirikiano, ili bunduki iliyoporwa iweze kupatikana.

“Tukio hilo lipo, ila nawaomba wananchi watoe ushirikiano wa kuipata bunduki hiyo kwani kitendo cha kupora silaha ni kosa ambalo haliwezi kuvumilika.

“Napenda pia kuwaamuru waliopora silaha hiyo, wairejeshe haraka kwani msako mkali utafanyika hadi itakapopatikana na wahusika kutiwa mbaroni.

“Narudia tena hili halikubaliki hata kidogo, yaani raia anamnyang’anya askari silaha
kali kama SMG!

“Hivi anapoichukua anaipeleka wapi, wairudishe haraka kwa sababu lazima watapatikana tu,” alisema mkuu huyo wa wilaya.

NA MOHAMED HAMAD-MTANZANIA KITETO

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post