SAKATA LA MISAADA YA MBUNGE WA CHADEMA KWA WAJAWAZITO KUKATALIWA HUKO BUKOBA LACHUKUA SURA MPYA



Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Mpoki Ulisubisya amesema misaada inayotolewa na watu mbalimbali kwa ajili ya kusaidia jamii ni lazima iwe imekidhi viwango vya ubora, hivyo haitakiwi kuangaliwa kwa vigezo vya dini, itikadi wala siasa.



Kauli hiyo ilitolewa jana na Katibu huyo wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisi kwake baada kituo kimojawapo nchini kukataa misaada iliyotolewa na Mbunge wa Bukoba Mjini (CHADEMA), Wilfred Lwakatare hivi karibuni. 



Dkt. Ulisubisya alisema hivi karibuni baadhi ya vyombo vya habari hapa nchini viliripoti kwamba misaada iliyotolewa na Mbunge huyo, katika baadhi vituo afya Zahanati kwa ajili ya wajawazito ilikataliwa. 



“Serikali ina sera ya kusaidia jamii hususan misaada inayotolewa kwenye huduma za afya, ambayo inakidhi viwango vya ubora kulingana Sheria , kanuni na taratibu za Mamlaka ya Chakula na Dawa(TFDA),” alisema Katibu Mkuu huyo. 



Hivi karibuni iliripotiwa kwamba baadhi ya wakuu wa vituo vya afya na zahanati katika Manispaa ya Bukoba, wamegoma kupokea msaada kwa ajili ya wajawazito uliotolewa na mbunge wa Chadema kwa madai ya kupewa maelekezo na Serikali.



Dkt. Ulisubisya amewataka watendaji wa afya wa vituo hivyo wasiangalie misaada hiyo kwa misingi ya dini, itikadi na kisiasa. 



Hata hivyo Katibu Mkuu huyo amewataka watu mbalimbali wenye lengo la kutoa misaada katika vituo vya afya kuhakikisha kwamba imekidhi viwango viliyowekwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA). 



Katika hatua nyingine aliyekuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dkt. Donan Mmbando amekabidhi ofisi hiyo kwa Katibu Mkuu huyo mpya.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Mpoki Ulisubisya (kulia) akikabidhiwa nyaraka muhimu na aliyekuwa katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dk Donan Mmbando.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post