Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

ULE MFUMO WA KUSINDIKIZA WAJINGA WAZIKWA DAR





WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, amefuta mfumo wa uwekaji matokeo wa ‘Grade Point Average (GPA) ulioanza kutumiwa na Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA) mwaka 2014.


Mfumo huo uliofuta mfumo uliokuwapo wa Divisheni, ulianza kutumika kwa kidato cha nne na sita na vyuo vya ualimu.

Inaelezwa kuwa mfumo huo ulianzishwa kujaribu kupandisha ufaulu baada ya kuonekana wanafunzi wengi walishindwa mitihani ya kidato cha nne, hasa mwaka 2013.

Mfumo huo ulilalamikiwa na wadau wa elimu waliodai kuwa ulikuwa unashusha kiwango cha elimu na kuwachanganya wanafunzi.

Akizungumza na waandishi wa habari Dodoma jana, Profesa Ndalichako, ambaye aliwahi kuwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), alisema baraza hilo limeshindwa kueleza sababu za kutumia mfumo huo badala yake limeishia kutoa utaratibu uliotumika tu.

“Kwa mamlaka niliyonayo chini ya kifungu cha 20 cha Sheria ya Baraza la Mitihani Tanzania, sura ya 107, naliagiza Baraza kufanya mapitio ya mfumo unaotumika sasa wa wastani wa alama (GPA) kwa lengo la kurudi kwenye mfumo wa awali wa Divisheni.

“Viwango vya ufaulu vizingatie azma ya nchi kuelekea kwenye uchumi wa kati na Tanzania ya viwanda,” alisema Profesa Ndalichako.

Kuhusu mtihani wa pili (Paper two), aliitaka NECTA kuufuta kwa watahiniwa wa kujitegemea.

Mtihani huo ulianzishwa kama alama ya maendeleo wakati ni mtihani wa mwisho.



“Wizara haiwezi kufikia azma ya kusimamia ubora wa elimu katika ngazi zote bila kuhakikisha viwango vya ufaulu vinawezesha kutoa wataalamu wenye stadi na maarifa badala ya kuwa na wahitimu wengi wenye vyeti lakini hawakidhi mahitaji ya soko la ajira,” alisema Profesa Ndalichako.

Januari 7 mwaka huu, Waziri Ndalichako alitembelea Necta na kuitaka itoe ufafanuzi wa kuacha kutumia mfumo wa divisheni na kutumia GPA.

Pia aliitaka itoe maelezo ya kuanzishwa kwa mtihani wa pili kwa watahiniwa wa kujitegemea.

Hata hivyo alisema jana kuwa maelezo yaliyotolewa yalikuwa yamejikita katika kueleza utaratibu badala ya sababu za kuutumia mfumo huo.

“Taarifa imebainisha kuwa uanzishwaji wa mfumo wa GPA ulitokana na maoni ya wadau bila kuwataja wadau husika na kueleza sababu walizotoa.

“Taarifa ya utafiti uliofanywea na Wizara ya Elimu haijataja idadi ya wadau waliojaza madodoso na wala haionyeshi mikutano ya kupata maoni ya wadau ilihusisha watu gani, ilifanyika wapi na lini,” alisema Profesa Ndalichako.

Kuhusu sababu kuwa NECTA ilipata maelekezo kutoka wa Wizara ya Elimu mwaka 2014, Profesa Ndalichako, alisema uchambuzi unaonyesha kuwa wizara ilikuwa imeelekeza baraza la mitihani liandae mfumo huo na kuuwasilisha kwa Kamishna wa Elimu upate kibali cha Serikali kabla ya kuanza kutumika.

“Hata hivyo, jambo hilo halikufanyika na badala yake Baraza hilo likaanza kutumia mfumo huo mwaka 2014. Nyaraka zilizowasilishwa hazionyeshi kama mapendekezo ya mfumo huo yaliwasilishwa kwa Kamishna wa Elimu,” alisema.

Alisema Baraza lilieleza faida ya kutumia GPA kuwa ni kueleweka kwake kwa urahisi na wadau jambo ambalo linapingana na maoni ya wadau yanayojitokeza kwenye vyombo vya habari, huku likishindwa kueleza udhaifu wa mfumo wa Divisheni.

“NECTA wameeleza kuwa mfumo wa GPA umerahisisha udahili wa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu (Collective Admission System- CAS) jambo ambalo si sahihi.

“Mfumo wa CAS ulianza kutumika Aprili 2010 wakati mfumo wa GPA ulianza kutumika mwaka 2014. Isitoshe huzingatia masomo mawili ya fani anayotarajia kusoma mwanafunzi siyo ufaulu wa jumla,” alisema.

Waziri alisema mfumo wa GPA ulikuwa bado kwenye majaribio hivyo haukupaswa kutumika kufanyia majaribio kwenye maisha ya watu.

Kuhusu sababu ya kuongeza mtihani wa pili kwa watahiniwa wa kujitegemea kama mbadala wa upimaji endelevu, alisema maelezo ya NECTA kuwa mtihani huo ni mbadala wa upimaji endelevu hayatekelezeki.

“Kitaalamu ‘paper two’ haiwezi kuwa alama ya maendeleo ya kila siku kwa kuwa inafanyika sambamba na mitihani mingine ya mwisho,” alisema Profesa Ndalichako.

Kwa sababu hiyo, Profesa Ndalichako, alisema kitendo cha baraza hilo kuingiza mfumo huo wa GPA katika marekebisho ya kanuni zake yaliyosainiwa na Waziri Oktoba 28 mwaka jana na kuchapishwa Novemba 6 mwaka jana kwenye gazeti la Serikali, ni kuonyesha kuwa mfumo huo ulianza kutumika bila kukamilika matakwa ya sheria.

“Mfumo wa GPA ulianza kutumika mwaka mmoja kabla haujaingizwa kwenye kanuni za mitihani,” alisema.

Akizungumzia hasara ya mfumo huo, Waziri Ndalichako alisema baadhi ya watahiniwa waliofaulu mitihani wanaonyesha kiwango kidogo cha maarifa kuliko kiwango cha ufaulu.

Alisema kuwapo daraja E kwenye alama za ufaulu wakati haihesabiki katika upangaji wa GPA kunawafanya watahiniwa waliopata E zote kwenye mitihani kujiona wako bora kuliko wenye D mbili na F zote, ambaye anahesabika kuwa amefaulu mtihani.

“Uwepo wa pointi za mfiko kwenye madaraja ya ufaulu kwa ngazi mbalimbali za elimu kunaleta mkanganyiko kwani inakuwa vigumu kueleza tafsiri ya madaraja hayo. Kwa mfano ‘Distinction’ ya kidato cha nne inaanza pointi 3.6 wakati ya ualimu inaanzia pointi 4.4,” alisema Waziri Ndalichako.

Pamoja na hatua hiyo aliyochukua, Profesa Ndalichako alisema bado Serikali haijaamua kuwachukualia hatua viongozi wa NECTA.

TAMONGSCO WAPONGEZA

Wakati huohuo, Chama cha Wamiliki wa Vyuo na Shule binafsi Tanzania (TAMONGSCO) kimepongeza hatua ya Profesa Ndalichako kufuta mfumo huo na kurejesha ule wa zamani wa Divisheni.

Katibu Mkuu wa Shrikisho hilo, Benjamin Nkonya aliliambia MTANZANIA jana kwamba mfumo wa GPA ulishusha madaraja ya ufaulu na kusaidia kusindikiza wanafunzi wengi zaidi kushindwa mitihani.

“Mfumo wa GPA ulikuwa mpango wa siasa, serikali iliona haijawekeza katika shule zake kwa kuweka maabara bora, kulipa vizuri walimu, kuweka mazingira mazuri hivyo kuchangia wanafunzi kufeli.

“Hivyo waliona wawadanganye wazazi kwa kuwaletea mfumo wasioujua huku wakitukwepa kutushirikisha wadau tukiwamo sisi.

“TAMONGSCO tunampongeza sana Waziri, Ndalichako na tunamshauri aweke mifumo endelevu ya kuzuia udhaifu wa aina hiyo kuingizwa katika sekta ya elimu katika siku za baadaye,” alisema Nkonya.
Chanzo-Mtanzania

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com