Viongozi wa Kitongoji cha Kasalazi, kilichoko katika Kijiji cha Kanyara, Kata ya Bulyaheke, wilayani Sengerema, Mkoa wa Mwanza, wanadaiwa kuwachapa fimbo hadharani wanawake wanaovaa nguo fupi zinazoonyesha baadhi ya sehemu zao za siri.
Pia, viongozi hao wanadaiwa kuwatoza faini ya Sh 20, 000 wanawake wanaokutwa na nguo hizo kama njia ya kuwafanya wasiendelee kuvaa nguo hizo.
Mmoja wa wasichana waliowahi kuchapwa na viongozi hao aliyejitambulisha kwa jina la Juliana Mafuru, alichapwa fimbo baada ya kufika kijijini hapo kwa lengo la kununua dagaa.
“Cha kushangaza ni kwamba, baada ya kufika katika kitongoji hicho, mgambo walinikamata na kunichalaza bakora mbele za watu nje ya boti niliyokuwa nimepanda.
“Pia waliamuru nivue suruali niliyokuwa nimeivaa na kuanza kuichana chana nyembe.
“Wakati wananifanyia hivyo, walitokea wasamalia wema ambao walinipatia shuka la kimasai ili niweze kujisitili, yaani waliniabisha kweli.
“Baadaye, walinipeleka kwenye ofisi ya kitongiji hicho na walinitoza faini ya shilingi 20,000, kisha wakaniachia,” alisema Juliana.
Nao wakazi wa kijiji hicho, Lafael Bitulo na Mariamu Chacha, walisema mwenyekiti wa kitongiji hicho na katibu wake, ndiyo vinara wa tabia hiyo kwa kuwa wamekuwa wakinufaika nayo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kitongoji hicho, Andrea Mkama, alikiri kuwachapa fimbo wanawake wanaovaa nguo fupi na zinazobana kwa mavazi wanayovaa ni ya udharirishaji.
Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kanyara, Lazoro Mgonzo, alithibitisha wanawake kuchapwa fimbo ingawa alisema ni kitendo cha udharirishaji.
Mkuu wa Wilaya Sengerema, Zainabu Terack alipoulizwa juu ya tukio hilo, alisema hana taarifa ingawa aliahidi kulifuatilia